Upinzani waitisha mgomo mkuu kupinga mauaji yanayolenga wanasiasa wa upinzani

Nchini Msumbiji, upinzani unaitisha mgomo mkuu leo Jumatatu, Oktoba 21 na maandamano nchini humo kukemea udanganyifu wakati wa uchaguzi uliopita wa Oktoba 9, ambao matokeo yake rasmi yanatarajiwa ndani ya siku chache. Lakini maandamano haya yanakuja siku mbili baada ya kuuawa kwa wanasiasa wawili wa mpinzani na mgombea urais Venancio Mondlane, hawa ni Elvino Dias, wakili wa Mondlane na Paulo Guamba, mwanachama wa chama cha Podemos. Mauaji haya yanaibua hisia mbalimbali.


Siku moja baada ya kifo cha wakili Elvino Dias, ambaye alikuwa akitayarisha rufaa ya kushtumu udanganyifu katika uchaguzi, Venancio Mondlane, mgombea urais, hana shaka kuhusu wahusika wa mauaji ya watu hawa wawili: "Waliofanya mauaji haya ni vikosi vya ulinzi na usalama. Vikosi vya usalama vya Msumbiji ndio walifanya hivyo. Tuna ushahidi. Damu ya vijana hawa wawili sasa inatiririka! Sisi sote tutaingia mitaani. Tutaandamana na mabango yetu. "

Hali tete

Uhalifu huu unafanyika katika mazingira ya mvutano baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, 2024, ambao matokeo ya mwisho yatatangazwa Oktoba 24, anakumbusha Lutero Simango, mkuu wa chama cha upinzani, MDM: "Mpaka suala hili litakapowekwa wazi, tunaweza kuhitimisha kuwa kitendo hiki cha uhalifu ni uhalifu wa kisiasa. "

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Pascoal Ronda, alitoa wito wa utulivu na kuagiza kufunguliwa kwa uchunguzi: "Serikali inazitaka taasisi zenye uwezo, hususan idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Polisi, kutoa mwanga haraka juu ya kesi hizi na kuwafikisha wahusika mbele vyombo vya sheria. "

Wawakilishi wa vyama vinavyolengwa

Msumbiji imekumbwa na mauaji kadhaa wakati wa uchaguzi, kama vile mauaji ya mwangalizi mmoja mwaka 2019 na mwandishi wa habari mwaka 2023, lakini hii ni mara ya kwanza kwa wawakilishi wa chama kulengwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii