Walimu, Madaktari wapigwa marufuku kusimamia miradi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ametaka Madaktari na Walimu kutokuwa wasimamizi wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa katika maeneo yao ya kazi huku akisisitiza kuwa sio taaluma yao na ni matumizi mabaya ya rasilimali watu.

Simbachawene ameyasema wakati akikagua ujenzi wa mradi wa vyumba viwili vya maabara venye thamani ya shilingi milioni 60 unaoendelea katika shule ya sekondari rudi iliyopo katika jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma, ikiwa ni ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Jimbo hilo.

Amesema, Uongozi wa Halmashauri zote nchini hasa Halmashauri ya Mpwapwa kuhakikisha inaachana utaratibu huo, iajiri wataalam wa fani ya ujenzi kwa ajili ya kusimamia miradi yote itakayokuwa ikitekelezwa katika Halmashauri hiyo ili iwe ya viwango vya ubora kama ambavyo baadhi ya Halmashauri zingine zinafanya.

“Kwa sasa majengo yetu yanajengwa na walimu na madaktari na badala ya kujengwa na wahandisi wa ujenzi, hili halikubariki hata kidogo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ajirini wataalamu wa ujenzi hata kwa ajira ya mkataba ili waweze kusimamia ujenzi haiwezekani miradi yetu isimamiwe na walimu na madaktari kwani wao sio Wahandisi wa majengo,” amesema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii