Kesi ya ulanguzi wa dawa za kulevya ilivyozima ndoto za Frida

Frida Ismail mwanamke wa miaka 35 kutoka Dar es salaam Tanzania japo anatabasamu la kupendeza , nyuma ya tabasamu hilo amebeba majuto na machungu
Hii inatokana na hali iliyomkuta wakati huo akiwa na umri wa miaka 28 alipokamatwa katika uwanja wa ndege huko Kilimanjaro nchini Tanzania na kile kilichotajwa kuwa ulanguzi wa madawa ya kulevya.
"Siku niliyokamatwa, ilikuwa katika uwanja wa ndege huko Kilimanjaro na kwa kweli ilikuwa wakati mgumu sana kwangu kuwa mikononi mwa polisi. Nililia sana , unajua sikuwahi kuingia polisi au hata kushtakiwa "anasema Frida.
Huo ulikuwa mwaka wa 2013 , Fridah anasema kwamba kama mwanamke kijana alikuwa na matamanio ya kuishi maisha yasiokuwa na bugudha , na alichukua uamuzi wa haraka ambao hakuzingatia athari zake .
Kulingana na mwanadada huyu wepesi wa kupata fedha nyingi ulimfunga macho kuona au kutafakari kwa kina kuhusu biashara alizokuwa anajihusisha nazo.
"Tuwe na uvumilivu na kupata ushauri sahihi pale tunapopitia magumu, nawahusia jamii nzima biashara haramu sio nzuri inaweza ikakupotezea dira ya maisha, kwa kuingia gerezani. Nawahusia bora ufanye biashara ndogo ndogo kujipatia kipato chako. Kuliko kuchukua uamuzi kama niliyoufanya nikaambulia maisha ya jela"anasema Fridah
Baada ya kukamatwa alifunguliwa kesi ya ulanguzi, na mahakama ilimpata na hatia na kumhukumu kifungo cha maisha . Alifungwa katika jela ya wanawake ya Karanga huko Moshi.
Fridah anasema kwamba alikamatwa mwaka wa 2013 , akakaa kama mahabusu miaka mitano na akaanza kutumikia kifungo chake mwaka wa 2017 ila alikata rufaa na kupewa uhuru wake 2019 .
"Ushahidi haukujitosheleza hivyo majaji waliamuru niachiliwe huru"anasema Fridah
Ila anapozungumzia matatizo na mahangaiko ya kukubali hali ya kwamba angeishi jela maisha, mwanamke huyu anazungumzia siku nyingi alizokaaa akilia mchana kutwa kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa nao .
Kukubali kwamba ni mfungwa ilikuwa ngumu sana kwake . Kila siku alivyoishi jela aliismfikiria binti yake wa miaka 5 aliyemuwacha nyumbani.
"Mimi nilifungwa maisha ila nilikaa miaka saba jela, na siku niliyokuwa jela kwa mara ya kwanza nililia sana maana mazingira yalikuwa mabaya sana na kitendo cha kulala saa tisa mchana mpaka kesho yake kilikuwa kinaniumiza ."Fridah anasema
Aidha alipokuwa akifikiria hasa wiki za kwanza gerezani, alitaja siku zilizojaa kiza kikuu asiweze kula, wala kupata hata lepe la usingizi. Anasema alikuwa haamini kwamba yuko jela na aliishi kwa maombi kila siku.
Fridah alizaliwa jijini Daresalam Tanzania , na kulelelewa katika maisha ya kawaida na watoto wengine . Kabla ya kuingia jela, anasema alikuwa amechumbiwa na mwanamume ambaye alikuwa ni Baba ya mtoto wake .
Anazungumza kuhusu huba Kati yake na Baba ya mwanae lililompa matumaini ya kuwa na ndoa naye katika siku za usoni.Asijue kwamba kukamatwa kwake na hatimaye kukaa gerezani kwa miaka saba kungekuwa sababu ya matumaini ya ndoa na mapenzi kukatika ghafla.
"Baada ya kutumikia kifungo, nilimkuta aliyekuwa mchumba wangu alioa na hata kujaaliwa watoto wawili, ni jambo ambalo liliniuma sana na kujeruhi moyo wangu mno "Fridah anasema
Mama huyu anasema kwamba kwa kuwa alifungwa mbali na Daresalam, hakufahamishwa kwamba mengi yalibadilika katika maisha yake nyumbani, kwani mtazamo wake na matumaini yake akiwa gerezani ilikuwa ni kwamba angemkuta mchumba wake akiwa anamsubiri. iIa mambo yalikuwa kinyume. Hali hio hadi sasa imemfanya asiweze kusonga mbele na mahusiano mapya miaka miwili baada ya kutoka jela.
"Sipo kwenye mahusiano kwa sasa maana moyo umejeruhiwa sana, labda baadaye Mungu akipenda "aliongeza mwandada huyo.
Anasema kwamba alimuwacha mwanae wa kiume na miaka 5 , na alipkuwa akielekea kuhudumia kifungo chake na ilimuumiza sana kila siku aliokuweko jela kufahamu kwamba mwanaye alikuwa hamuoni.
Hatahivyo wazazi wake Fridah walichukua majukumu ya kumlea mjukuu wao..
Na alipokamilisha kifungo chake jela alirudi nyumbani na kumkuta bintiye akiwa na umri wa miaka 12 , hatua iliomfanya kuanza safari mpya ya uponaji na kufahamiana tena.
"Wazazi wangu walijisikia vibaya sana kwa kuwa walikuwa hawajui kuhusu sababu za kukamatwa kwangu na baadaye kuhukumiwa, "anasema Fridah maisha baada ya kifungo gerezani yalijawa na upweke kwani alikuwa akiwaogopa watu.
"Nilikuwa naogopa kukaribiana sana na watu, jinsi watu wanavyokuchukulia sio jinsi unavyojichukulia, saa zengine watu wanakuona kama mkosaji kumbe hapana, kumbuka gerezani ni sehemu ya urekebishaji. Kuna watu wanakutenga na pia marafiki wanakuona kama mkosefu wa siku zote "Fridah anasema
Kwasasa ana mpango wa kufungua shirika huru la kutetea haki za wanawake , watoto na hata wanaume wafungwa akidai kwamba wanapitia wakati mgumu wakiwa gerezani na hata baada ya kuachiliwa huru.
"Daima mtu hawezi kuwa mkosaji, wengi ni wale wanabadilika baada ya kuwa gerezani, ila wanapotoka nje kunakuwa na ugumu kutangamana na raia ambao wanawatenga wafungwa hasa wanawake. Kwa hiyo inakuwa ni muhimu sisi kutumia mafunzo tuliyopewa gerezani kwa mfano kuoka mikate , kushona na mambo mengine"aliongezea.
Yote tisa, kumi mwanadada huyo anajipiga kifua kama mfungwa aliyepevuka na kufunguka macho akiwa gerezani, anasema mbali na kwamba mtazamo wake wa maisha ulibadilika anashukuru wazazi wake kwa kusimama na yeye na pia watu wenye imani sawia na yake .
Anasema kwamba mafunzo ya kuoka mikate,ushonaji fulana na hata batiki, ni masomo ambayo anayategemea katika kuinua maisha yake .

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii