BENKI KUU YA TANZANIA YATOA MAFUNZO YA KUTAMBUA NOTI HALALI KWA WATU WA MAKUNDI MAALUMU

Katibu Mtendaji wa Shirika la maendeleo ya jamii na viziwi (DCPO),Jafari Shabani akizungumza kuhusiana na mafunzo hayo.


Benki kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya kutambua noti halali kwa watu wa makundi  maalumu wakiwemo wasioona,wenye ulemavu wa macho na viungo.

Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Meneja Msaidizi  Sarafu, Joyce Saidimu ,alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuyawezesha makundi hayo kupata uelewa wa kutosha wa kuzijua alama za usalama kwenye sarafu ili kuweza 

kugundua fedha halali kwani ni makundi ambayo yamekuwa yakisahaulika katika maswala  mbalimbali.

Saidimu alisema kuwa,wameona umuhimu mkubwa wa kutoa mafunzo kwa makundi hayo  ili waweze kuzitambua fedha halali na kuepukana na matumizi ya fedha bandia kutokana na 

changamoto walizonazo, na hatimaye kuweza kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili na wengine ambao hawajafikiwa waweze kufikiwa kupitia wao. 

“Sisi kama Benki ni utaratibu wetu kutoa mafunzo kama hayo mashuleni, sokoni na kwenye maeneo mbalimbali ya biashara, ila kwa awamu hii tumeamua kutoa elimu kwa watu wa  makundi maalumu ili waweze kupata uelewa wa kutosha na kuzitambua noti halali.

“Mafunzo haya yatakuwa endelevu na tutakuwa tukiyatoa mara kwa mara ili waweze kupata uelewa wa 

kutosha juu ya maswala haya na kuepuka kushikishwa fedha bandia kwani tayari wana uelewa  wa kutosha”, alisema Saidimu.

Aidha wameweza pia kutoa mafunzo ya namna sahihi ya kutunza fedha kwa ajili ya matumizi  yao huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa kufundisha wenzao namna ya kutunza fedha .

Akizungumza baada ya mafunzo hayo ,Katibu Mtendaji wa shirika la maendeleo ya jamii na viziwi (DCPO),Jafari Shabani alisema kuwa ,waliomba kupatiwa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu kutokana na changamoto mbalimbali walizokuwa wakikabiliana nazo katika kuzitambua noti bandia na halali,ambapo jumla ya watu wenye mahitaji maalumu 70 

wameweza kupatiwa mafunzo hayo. 

Jafari alisema kuwa, watu hao wenye mahitaji maalumu walikuwa wakikabiliwa na  changamoto hiyo na hata kupelekea wengi wao kupelekwa katika vyombo vya usalama pindi wanapokutwa na noti bandia kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya utambuzi wa 

alama za usalama kwenye sarafu. 

Kwa upande wake ,Mshiriki wa semina hiyo Emmanuel Benjamini ameishukuru Benki Kuu kwa mafunzo hayo kwani hapo awali alikuwa akishikishwa sana noti bandia kutokana na biashara yake ya kuendesha Bajaji ila kutokana na elimu hiyo sasa wataweza kuchukua tahadhari mapema.

Aidha aliomba mafunzo hayo kuwa endelevu huku akiomba serikali kutoa mafunzo zaidi kwa watu wenye ulemavu kwani itasaidia sana kuona wanashirikishwa na kuondoa dhana ya kutatuliwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii