China yalegeza masharti ya kudhibiti maambukizi ya corona

China imelegeza taratibu za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kwenye baadhi ya maeneo lakini imesisitiza kwamba itasonga mbele na sera yake inayolenga shabaha ya kuzuia maambukizi yote. China imesisitiza hayo baada ya baadhi ya waandamanaji wanaopinga sera hiyo inayowazuia mamilioni ya watu majumbani mwao, kumtaka rais wa nchi hiyo Xi Jinping ajiuzulu.

Hata hivyo serikali ya China haijasema lolote juu ya malalamiko ya waandamaji dhidi ya chama tawala cha kikomunisti. Na wala hakuna kauli rasmi iliyotolewa na serikali juu ya watu wengi waliotiwa ndani baada ya polisi kutumia vipulizo vya pilipili kuwashambulia waandamanaji kwenye mji wa Shanghai na kujaribu kuwabana waandamanaji kwenye miji mingine ikiwa pamoja na mji mkuu, Beijing. Hadi leo Jumatatu China imeorodhesha watu wapatao 40,347 ambao wameambukizwa virusi vya corona.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii