Baadhi ya waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde usharika wa Ruanda, wanaomuunga mkono Askofu Edward Mwaikali aliyeondolewa katika kanisa hilo, wamesusia ibada kwa kile kinachoendelea juu ya mgogoro katika kanisa hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Askofu Mwaikali ambaye sasa ametangaza kuhamia Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki (KKAM), kukabidhi baadhi ya mali za kanisa hilo.
Katika ibada ya leo Jumapili Juni 19, kanisani hapo iliendeshwa na Askofu mstaafu, Dk Israel Peter Mwakyolile ambaye amesisitiza kutubu akisema kuwa wachungaji wametenda dhambi kubwa na waathirika ni waamini ambao hawana hatia.
"Mungu atusamehe sana, Dk Mwaikali na sisi wengine, wachungaji wametenda dhambi kubwa badala ya kutengeneza wamebomoa kwani tumepoteza watu wengi tunaporudi nyumbani tutafakari upya," amesema Dk Mwakyolile ambaye ametokwa na chozi wakati akizungumza madhabauni.
baadhi ya ya waamini wakiwa baadhi wamekaa kwenye viti nje ya kanisa wengine wakiwa wamesimama kwa makundi makundi wakionekana kupanga mipango yao.
Pia kama haitoshi, wapo ambao walifika kanisani hapo lakini ni kama hawakuelewa mwenendo na kuamua kuondoka kabla ya ibada kumalizika.