kina Mdee kortini tena leo

Waliokuwa wanachama 19 wa Chadema, akiwamo Halima Mdee wanaingia katika mchuano na chama hicho wakati wa usikilizwaji wa pingamizi dhidi ya maombi ya amri ya kudumisha hali ilivyo (kulinda ubunge wao).

Mdee na wenzake 18 wamefungua maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema (iliyosajiliwa), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakiomba ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa chama cha Chadema.

Sambamba na maombi hayo ya ridhaa namba 27 ya mwaka 2022, pia wamefungua maombi namba 16 ya mwaka 2022 kwa ajili ya kupata amri ya mahakama kudumisha hali ilivyo kwa sasa.

Amri hiyo inalenga kuizuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Spika, kutekeleza uamuzi huo wa Chadema kuwavua uanachama.

Maombi hayo yote yalitajwa mahakamani juzi, lakini Chadema wakaibua pingamizi dhidi ya maombi hayo ya zuio.

Katika pingamizi lao, Chadema wanapinga usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio wakidai kuwa kiapo kinachoyaunga mkono kina kasoro za kisheria, huku wakibainisha hoja tatu za kasoro hizo.


Pamoja na mambo mengine, Chadema kupitia kwa jopo la mawakili wake linaloongozwa na Peter Kibatala inadai kiapo hicho kina kasoro kutokana na kuingizwa mambo yasiyopaswa kuwamo.

Mambo hayo ni hoja, maoni na mambo ya uvumi, masuala ambayo ni kinyume cha matakwa ya kisheria, inayoelekeza kuwa taarifa za kwenye kiapo ziwe ni za ufahamu wa mla kiapo na kusiwe na maoni, mapendekezo au taarifa za uvumi.

Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitoa amri ya kudumisha hali ilivyo kwa sasa kuhusu hadhi ya ubunge wa kina Mdee hadi leo wakati maombi hayo ya zuio yatakaposikilizwa.

Tayari jana Chadema waliwasilisha mahakamani kiapo kinzani kujibu maombi hayo ya kina Mdee wanaowakilishwa na mawakili Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya na Edson Kilatu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii