Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi kesho inatarajia kuendelea kuunguruma baada ya mapumziko ya mwisho wa juma.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Joachim Tiganga, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Jumatatu Novemba 15, 2021 inatarajiwa kuendelea kuunguruma kwa kuanza na kiporo cha mapingamizi yaliyotawala na kutikisa katika kesi hiyo.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 ni Halfan Bwire Hassan (mshtakiwa wa kwanza) na Mohamed Abdillahi Ling’wenya (mshtakiwa wa tatu).
Washtakiwa hao watatu walikuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), katika kikosi cha Makomandoo 92 KJ, Ngerengere Morogoro ambao wanadaiwa kuachishwa kwa sababu za kinidhamu.
Wote wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita, mawili ya kula njama ili kutenda vitendo vya kigaidi, kwa washtakiwa wote, vitendo vinavyodaiwa kutishia amani na usalama wa wananchi kwa lengo la kusababisha hofu kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.