Marehemu Wakili Alute Mughwai Lissu aliwahi kushawishiwa na familia yake kuachana na uwakilishi wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Arusha, iliyosababisha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema, kuvuliwa ubunge.
Akisoma wasifu wa marehemu Alute leo kijijini Mahambe wilayani Ikungi mkoani Singida, Wakili Ikoti Lissu amesema kuwa wakati huo Lema alimweleza Tundu Lissu amshawishi Alute asisimamie kesi hiyo kwa niaba ya wanachama wa CCM.
Hata hivyo, amesema Alute alikataa ushauri huo na kuamua kuendelea na jukumu lake la kuwatetea wanachama hao mahakamani licha ya shinikizo alilokuwa akipata kutoka kwa familia yake.
Ameongeza kuwa msimamo huo ulidhihirisha namna marehemu Alute alivyokuwa akizingatia misingi ya taaluma yake ya uwakili na kutanguliza wajibu wa kumtetea mteja bila kujali itikadi za kisiasa.