Rais Samia Aagiza Wakulima Wadogo Wanufaike na Shamba la Serikali Mbarali, Mbeya

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameonya dhidi ya watu wanaoweza kutumia nguvu zao za kiuchumi au nafasi zao kujinufaisha kupitia mpango wa Serikali wa shamba la Highland Estate lililopo wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, badala ya kuwawezesha wakulima wadogo waliokusudiwa kunufaika.

Ndejembi amesema fedha zinazotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kulirejesha shamba hilo chini ya usimamizi wa Serikali zinapaswa kuwanufaisha wakulima halisi, na si kuwa fursa kwa watu wachache wenye uwezo wa kifedha kujipatia manufaa binafsi.

Akizungumza wakati wa ziara yake Rujewa mkoani Mbeya, ambako aliwasilisha salamu za Rais Samia, Makamu wa Rais amesema Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya malipo ya shamba hilo lenye takribani ekari 6,000, ambalo limefanyiwa uthamini wa Shilingi bilioni 30.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wadogo wanapata fursa ya kukodi maeneo ya shamba hilo kwa gharama nafuu, tofauti na gharama za kati ya Shilingi 600,000 na 700,000 kwa ekari zinazotozwa katika baadhi ya maeneo mengine.




Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii