Watoto 29 wafa baada ya paa la shule kuporomoka

Watu wasiopungua 29, akiwemo mwalimu mmoja wa kike, wamefariki baada ya paa la shule kuporomoka katika mji wa Peshawar, kaskazini magharibi mwa Pakistan. Zaidi ya watu 40 wamejeruhiwa, huku watoto wengine wakihofiwa kukwama chini ya vifusi.
Kwa mujibu wa maafisa wa uokoaji, tukio hilo limetokea mapema leo Alhamisi, wakati watoto wenye umri usiozidi miaka 12 walipokuwa madarasani. Chanzo cha kuporomoka kwa paa hilo bado hakijafahamika.

Msemaji wa hospitali walikopelekwa majeruhi, Mohamed Asim, amesema baadhi ya watoto wamejeruhiwa na nondo za chuma na hali zao ni mbaya. Maafisa wanaonya kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.

Makumi ya waokoaji, wakisaidiwa na mashine nzito pamoja na watu waliojitolea, wanaendelea kuondoa vifusi kuwatafuta waliokwama. Vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti kuwa zaidi ya watoto mia moja walikuwa shuleni wakati paa lilipoporomoka.

Picha za televisheni zimeonyesha wazazi wakikimbia barabarani kwa hofu, huku magari ya wagonjwa yakiwaharakisha watoto hospitalini.

Afisa wa polisi Mian Saeed amesema mmiliki wa shule hiyo amekamatwa na uchunguzi umeagizwa kubaini kilichosababisha tukio hilo. Juhudi za uokoaji zinaendelea, huku maafisa wakihofia kuwa watoto wengine wengi bado wako chini ya vifusi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii