PGMOL Yakubali VAR Ilikosea Bao la Haaland Dhidi ya Man United

Chombo cha Waamuzi wa kulipwa nchini Uingereza (PGMOL) kimewasiliana rasmi na klabu ya Manchester United na kuomba radhi baada ya kukiri kuwepo kwa “makosa ya kimaamuzi” katika goli la mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, lililoamua Dabi ya Manchester iliyochezwa jana usiku.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulifikia hatua ya sintofahamu katika dakika ya 60, wakati Haaland alipofunga goli pekee lililoipa Manchester City ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United katika dimba la Old Trafford.

Awali, mwamuzi wa pembeni alinyanyua bendera kuashiria kuwa Haaland alikuwa katika nafasi ya kuotea (offside), hivyo goli hilo likakataliwa.

Hata hivyo, mfumo wa usaidizi wa waamuzi kwa njia ya video (VAR) uliingilia kati na kuufanyia mapitio uamuzi huo. Baada ya kuchora mistari ya offside na kupitia picha za marudio, VAR ilibaini kuwa Haaland hakuwa ameotea, kutokana na nafasi ya beki wa Manchester United, Patrick Dorgu.

Lakini tatizo lilijitokeza katika hatua ya kutathmini ushawishi wa kiungo wa Manchester City, Enzo Fernández, ambaye alikuwa katika nafasi ya kuotea wakati mpira ukipigwa.

Fernández aliruka juu akijaribu kuucheza mpira kwa kichwa huku akiwa anagombea nafasi na beki wa Manchester United, Lisandro Martínez.

Kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa kuwa aliingilia mchezo na kuathiri uwezo wa Martínez kucheza au kutetea mpira.

Hata hivyo, VAR ilishindwa kutathmini kikamilifu tukio hilo na kuzingatia tu nafasi ya Haaland, jambo ambalo baadaye lilionekana kuwa sehemu ya kosa la kimaamuzi.

PGMOL imekiri kuwa VAR ilipaswa kuzingatia pia kitendo cha Fernández na ushawishi wake kwa Martínez kabla ya kuthibitisha goli hilo.

Kutokana na hilo, PGMOL imewasiliana na Manchester United na kuomba radhi kwa kosa hilo, huku tukio hilo likiendelea kuibua mjadala kuhusu matumizi ya VAR na namna waamuzi wanavyotathmini matukio ya kuotea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii