Kenya imejiunga na nchi zingine za Afrika kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa lililoanzisha Novemba 27 kama Siku ya Kimataifa ya kutokomeza ndoa za utotoni na kulazimishwa.
Azimio hilo limepitishwa kwa kauli moja na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likilenga kuhimiza hatua zaidi kukomesha ndoa za utotoni na kuimarisha ulinzi wa watoto, hususan wasichana.
Kenya ni miongoni mwa nchi 20 za Afrika zilizoshirikiana kudhamini azimio hilo, pamoja na Gambia, Ghana, Guinea, Liberia, Rwanda, Uganda na Zambia.
Hatua hiyo inaweka suala la ndoa za utotoni katika ajenda ya kimataifa, wakati huu mataifa yakiharakisha utekelezaji wa Malengo Endelevu yanayohusu elimu, usawa wa kijinsia, afya na ulinzi wa watoto.
Azimio hilo linazitaka serikali kuimarisha sheria, kuboresha upatikanaji wa elimu na kuongeza ulinzi kwa wasichana walio katika hatari ya kuolewa wakiwa watoto.