Miezi minne baada ya kuanza kwa janga la Ebola, kiwango cha maambukizi bado hakijafikiwa, nchini DRC. Hii ilitangazwa na shirika la afya la Umoja wa Afrika, Africa CDC, siku ya Alhamisi, Septemba 17, wakati wa mkutano na waandishi wa habari. Uchambuzi huu unatofautiana na ule wa mamlaka ya Kongo, ambao walibainisha wiki iliyopita kwamba kilele hicho kilikuwa kimefikiwa katikati ya mwezi Agosti.
Nchini DRC, idadi ya wagonjwa wa Ebola waliothibitishwa sasa imefikia 7,404, ikiwa ni pamoja na vifo 3,577 na wagonjwa wa virusi hivyo waliopona ni 1,776. Kulingana na Dkt. Wessam Mankoula, maendeleo yamepatikana katika baadhi ya maeneo ya afya, lakini bado hayajaenea hadi maeneo yote yaliyoathiriwa. "Tunapozungumzia kilele, ni muhimu kuelewa kwamba kunaweza kuwa na vilele kadhaa wakati wa janga," anaelezea mkuu wa mwitikio wa dharura katika Afrika CDC. "Kunaweza kuwa na ongezeko la idadi ya wagonjwa, ambao unadhibiti, kisha hali inatulia, kunaweza hata kuwa na upungufu kidogo. Lakini usipodumisha udhibiti huu baada ya muda, idadi ya wagonjwa inaweza kuongezeka tena."
"Hivyo ndivyo ilivyotokea mwishoni mwa mwezi Julai: kulikuwa na kipindi cha utulivu, kikifuatiwa na ongezeko jipya, anaendelea kueleza, kwa hiyo ndiyo, kuna maendeleo katika baadhi ya maeneo ya afya, lakini hatupaswi kuwa na matumaini kupita kiasi. Katika maeneo saba ya afya, hakujakuwa na visa vipya kwa siku 42. Katika maeneo sita, hajaripotiwa kisa kipya tangu siku 21 zilizopita" .
"Lakini bado kuna maeneo 49 ya afya ambapo kuna maambukizi mapya. Maeneo haya yanawakilisha karibu 80% ya maeneo ya afya yaliyoathiriwa. Kwa hivyo ni mapema mno kusema kwamba mlipuko huu unadhibitiwa."