Wezi waiba jeneza, walitelekeza karibu na kanisa

WATU wasiojulikana wameiba jeneza katika ofisi ya biashara iliyopo Kijiji cha Mbweera, Kata ya Masama, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, kabla ya kulitelekeza katika barabara ya kuingilia Kanisa la KKKT, Usharika wa Masama Kati.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema lilitokea usiku wa kuamkia jana.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wezi hao waliiba jeneza hilo, kisha walilitelekeza kwenye njia ya kuelekea kanisani baada ya kuona mwanga wa tochi ukiwaelekea.

“Watu hao waliingia katika eneo la biashara na kuchukua jeneza. Baada ya kuona mwanga wa tochi ukiwaelekea, walitelekeza jeneza hilo katika njia ya kuingilia kanisani,” amesema Maigwa.

Amesema katika tukio hilo hakuna mali nyingine iliyoibwa wala mtu yeyote aliyepata madhara.

Kamanda Maigwa amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wahusika waliingia katika ofisi hiyo kwa kufungua mlango na kulichukua jeneza hilo.

Amesema mmiliki wa eneo hilo alieleza kuwa alikuwa na utaratibu wa kufunga mlango kwa kuuegesha bila kutumia kufuli, akiamini kuwa hakuna mtu ambaye angeweza kuiba jeneza.

“Uchunguzi wa kina unaendelea ili kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi,” amesema.

Kamanda Maigwa amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kiusalama kwa kuhakikisha milango ya nyumba, maduka, ofisi na maeneo mengine inafungwa kwa kufuli, hasa nyakati za usiku.

Amesema wananchi hawapaswi kubeza usalama wa mali kwa kuangalia aina au thamani yake, bali wanapaswa kuhakikisha kila eneo linafungwa na kulindwa ipasavyo, ili kuzuia vitendo vya uhalifu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii