JUHUDI za uokoaji zinaendelea nchini Nepal na China, baada ya mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo yaliyotokea wiki iliyopita, kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 huku wengine 4,800 wakiwa hawajulikani walipo.
Aidha, mtoto wa miaka sita ameokolewa akiwa hai siku nne baada ya maafa na baadaye kukutanishwa tena na wazazi wake.
Maafa hayo, yaliyosababishwa na kuporomoka kwa sehemu ya barafu katika milima ya Himalaya, huku vikosi vya uokoaji vikitumia helikopta, magari makubwa na mbwa wenye uzoefu katika shughuli za uokozi.
Waokoaji nchini Nepal, wakisaidiwa na wataalamu kutoka China, India na Korea Kusini, wanaendelea na juhudi za kuwatafuta mamia ya watu wanaoaminika kukwama ndani ya mahandaki ya mabwawa ya umeme katika wilaya za Rasuwa na Nuwakot.
Takribani wafanyakazi 933 wanaaminika kuwa wamekwama katika jumla ya miradi 11 ya umeme, huku zaidi ya watu 300 wakihofiwa kunaswa ndani ya handaki moja katika mradi wa Upper Trishuli-1. Hadi leo, miili mitatu imepatikana kutoka katika vichuguu viwili, lakini sehemu nyingine bado zimefunikwa na matope mazito.
Maelfu ya watu wameachwa bila makazi, barabara na madaraja yameharibiwa vibaya, huku serikali ya Nepal ikikadiria kuwa gharama za ujenzi mpya zinaweza kufikia mabilioni ya Dola za Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Nepal, Shisir Khanal, amesema wananchi wa nchi hiyo ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, mamlaka za uokoaji likiwamo Jeshi la Polisi nchini Nepal, zinasema changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa ni namna eneo lenyewe lilivyo na kwamba rasilimali walizonazo pia hazitoshi.
Wakati huo huo, upande wa Tibet nchini China, watu 16 wamethibitishwa kufariki na zaidi ya 500 hawajulikani waliko. Serikali ya China imetuma zaidi ya waokoaji 2,000 na kutoa mamilioni ya dola kwa ajili ya shughuli za uokoaji na misaada ya kibinaadamu.
Wataalamu wanaonya kuwa ongezeko la joto duniani linalosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi linazidisha kasi ya kuyeyuka kwa barafu katika milima ya Himalaya, na hivyo kuongeza hatari ya kutokea majanga mara kwa mara.