Lukwago na Besigye warejeshwa tena hospitalini

Idara ya huduma za magereza nchini Uganda, imethibitisha kuwa wanasiasa wa upinzani wanaoendelea kuzuiliwa Dkt Kizza Besigye na Meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago, wamerejeshwa tena hospitali baada ya afya zao kuzorota.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa idara hiyo, Frank Baine, imethibitisha washukiwa hao kupelekwa hospitali lakini akakanusha madai kuwa hali zao ni mbaya.

Baine amesema lkilichofanyika kinafuatia agizo la mahakama na tathmini ya madaktari wanaowatibu wanasiasa hao ambapo walipendekeza warejeshwe hospitali kwa uangalizi zaidi.

Kauli ya Magereza imekuja baada ya Agosti 28, mke wa Besigye, Winnie Byanyima kudai kuwa mume wake alikuwa kwenye hali mbaya na kwamba yuko hospitali kwa uangalizi maalumu, Winnie akidai bado mwanasiasa huyo hawezi kuzungumza.

Tangu alipoanguka na kuzirai mahakamani majuma kadhaa yaliyopita akipinga kutokupewa haki ya kuchagua mawakili wakumtetea anaowaamini, afya ya Besigye haijatengamaa, mke wake akitaka aruhusiwe kupelekwa Geneva kwa matibabu zaidi.

Besigye pamoja na mwenzake Obeid Lutale na kapteni wa jeshi Denis Oola, wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini makosa wanayodaiwa waliyafanya kati ya mwaka 2023 na 2024.

Lukwago mmoja wa mawakili wakuu wa Besigye alikamatwa kwa tuhuma kama hizo huku wakili kiongozi ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa sheria wa Kenya, Martha Karua, akipigwa marufuku kuingia nchini humo, hali iliyosababisha Besigye kuwakataa mawakili aliochaguliwa na Serikali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii