Uasi ulioitikisa serikali ya kijeshi Niger ndani ya saa 24

Mji mkuu wa Niger, Niamey, ulirejea katika hali ya utulivuJumapili baada ya takriban saa 24 za mapigano yaliyoutikisa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo. Wanajeshi waliokuwa na malalamiko dhidi ya serikali waliasi na kupambana na vikosi vilivyo waaminifu kwa kiongozi wa junta, Jenerali Abdourahamane Tchiani.

Uasi huo umetajwa kuwa mojawapo ya vitisho vikubwa zaidi kwa serikali ya kijeshi tangu ilipotwaa madaraka kwa mapinduzi ya Julai 2023. Mapigano makali yaliendelea kuanzia usiku wa kuamkia Jumamosi hadi mwishoni mwa siku hiyo, huku milio ya risasi na milipuko ikisikika katika maeneo muhimu ya mji mkuu.

Kitovu kikuu cha mapigano kilikuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani, ambako pia kuna kambi muhimu ya Jeshi la Anga inayojulikana kama Base 101. Eneo hilo vilevile linahifadhi makao makuu ya kikosi cha Russia Africa Corps nchini Niger.

Milio mingine ya risasi ilisikika karibu na ikulu katika wilaya ya Plateau. Huko, kundi jingine la wanajeshi waasi lilikabiliana na walinzi wa rais na vikosi vingine vilivyobaki waaminifu kwa serikali ya kijeshi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii