Kufuatia mazungumzo kati ya Walibya huko Tunis siku ya Alhamisi, Agosti 20, 2026, yaliyowezeshwa na Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), Sehemu za Mashariki zinazotawaliwa na Jenerali Field Marshal Haftar na zile za Magharibi zinazotawaliwa na serikali ya umoja wa kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na jumuiya ya kimataifa, zinaonekana kufikia makubaliano ya mpango wa kisiasa utakaoruhusu nchi hiyo kuandaa uchaguzi wa rais na wa wabunge mnamo mwaka wa 2027.
Hata hivyo, makubaliano haya yanabaki kuwa dhaifu kutokana na mvutano na mgawanyiko ndani ya nchi hiyo, ambayo haijafanya uchaguzi wa bunge tangu 2014 na haijawahi kufanya uchaguzi wa rais.
Mshauri mkuu wa masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati katika serikali ya Trump amepongeza maendeleo yaliyofikiwa na walioshiriki mazungumzo kutoka Libya kuelekea makubaliano ya sheria za uchaguzi. Mazungumzo hayo yanayofanyika Tunis kati ya wawakilishi wa Mashariki na Magharibi mwa Libya kwa sasa bado ni ya siri kulingana na Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), ambao umeonya dhidi ya taarifa potofu zinazosambaa kuhusu makubaliano hayo.
Hadi sasa, machache sana yanajulikana kuhusu mchakato huu isipokuwa kwamba mazungumzo yanahusu mwongozo uliokubaliwa mnamo mwezi Juni kwa ajili ya kuandaa uchaguzi wa rais na wabunge mwaka wa 2027. Lengo la majadiliano haya ya kwanza lilikuwa ni kuainisha mfumo wa kisheria wa chaguzi hizo pamoja na kuunda Baraza la Tume Kuu ya Kitaifa ya Uchaguzi.
Mara tu baada ya kutangazwa kwa makubaliano kufanywa katika vyombo vya habari vya Libya, mkuu wa Baraza la Rais, Mohamed Al-Menfi, huko Tripoli, alielezea wasiwasi kuhusu mbinu zilizotumika katika mpangilio huu na ukosefu wa uwazi. Mchakato wa Umoja wa Mataifa kwa kweli unakosolewa magharibi mwa Libya, haswa na makundi ya kisiasa ambayo pia yalikutana Tunis Jumanne, Agosti 18, siku mbili kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa.