Hofu zatawala ZImbabwe kufuatia mapendekezo ya mabadiliko ya katiba

Hofu inaongezeka miongoni mwa upinzani nchini Zimbabwe kufuatia mapendekezo ya mabadiliko ya katiba yanayodaiwa kuimarisha zaidi mamlaka ya chama tawala cha Zanu-PF.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, bunge linaweza kupewa mamlaka ya kumchagua rais badala ya wananchi, huku muda wa urais ukipendekezwa kuongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.

Aidha, mabadiliko hayo yanaweza kumruhusu Rais wa sasa, Emmerson Mnangagwa, kuendelea madarakani hadi mwaka 2030 badala ya kumaliza muda wake mwaka 2028.

Mwanasiasa mkongwe wa upinzani na aliyewahi kuwa waziri wa fedha, Tendai Biti, ameelezea hatua hiyo kama “mapinduzi ya polepole” yanayoendelea nchini humo.


Hata hivyo, Zanu-PF imetetea vikali mabadiliko hayo, ikisema yanaweza kusaidia kupunguza gharama za uchaguzi na kuondoa migogoro ya kisiasa.

Afisa wa chama hicho, Patrick Chinamasa, amesisitiza kuwa hakuna kinachokizuia chama hicho kubadili mfumo wa uongozi.

Mapendekezo hayo pia yanajumuisha kuahirishwa kwa uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika mwaka 2028 hadi 2030, pamoja na kuanzishwa kwa mfumo mpya ambapo bunge jipya litamchagua rais ajaye.

Mvutano mkubwa umejitokeza kati ya wafuasi wa Zanu-PF na upinzani, huku vikao vya hadhara vilivyofanyika jijini Harare vikishuhudia maelfu ya wananchi wakitoa maoni yao—wengine wakiunga mkono, na wengine wakipinga mabadiliko hayo.

Hata hivyo wachambuzi wanasema mjadala huu unaashiria mgawanyiko mkubwa wa kisiasa nchini humo, huku hatima ya mabadiliko hayo ikitarajiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa mustakabali wa demokrasia ya Zimbabwe.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii