Bao pekee alilofunga Axel Tuanzebe katika mchezo wa mchujo dhidi ya timu ya Taifa ya Jamaica limetosha kuirudisha DR Congo katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Juni mwaka huu Marekani, Canada na Mexico.
Imepita miaka 52 tangu mara ya mwisho DR Congo iliposhiriki michuano hiyo mwaka 1974 wakati huo ikijulikana kama Zaire.
Katika michuano hiyo iliyokuwa ikifanyika Ujerumani, DR Congo ilitolewa katika hatua ya makundi huku ikikumbana na kipigo cha fedheha cha mabao 9-0 dhidi ya Yugoslavia.
Katika mchezo wa mchujo uliopigwa usiku wa kuamkia leo huko Guadalajara, Mexico ilishuhudiwa DR Congo wakikata tiketi ya pili kucheza fainali za Kombe la Dunia katika muda wa ziada baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Vijana wa kocha, Sebastian Desabre walionesha hali ya kujituma muda wote wakishambulia na kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao hao kutokea Marekani Kaskazini.
Hata hivyo, katika dakika ya 100 ya mchezo Tuanzebe aliihakikishia DR Congo tiketi ya kucheza Kombe la Dunia la mwaka huu baada ya kufunga bao pekee kwa kichwa kilichojaa moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Jamaica, Andre Blake akiwa hana cha kufanya.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime