Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata madereva wanne kwa kosa la kuendesha vyombo vya moto wakiwa chini ya ushawishi wa ulevi katika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Alex Mkama, ukamataji huo ulifanyika Desemba 25 mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro na Wilaya ya Kilombero, wakati wa operesheni maalum za kudhibiti usalama barabarani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Alexander Mapunda (45) mkazi wa Foresti alikamatwa akiendesha gari aina ya Nissan X-Trail akiwa na kiwango cha ulevi cha 667.4 mg/100ml.
Ambapo Theodory John (33) mkazi wa Mafiga alikamatwa akiwa anaendesha Toyota Premio akiwa na kiwango cha ulevi cha 171.4 mg/100ml huku Bikayi Semione (31) mkazi wa Ifaragha akikamatwa akiendesha Toyota Hiace akiwa na kiwango cha ulevi cha 408.9 mg/100ml.
Aidha Johana Nkoa (28) mkazi wa Modeka alikamatwa akiendesha pikipiki aina ya Haojue akiwa na kiwango cha ulevi cha 776.8 mg/100ml.
Katika tukio lingine Polisi walimkamata Hussein Rashid (40) mkulima mkazi wa Ifakara katika Kata ya Katindiuka Wilaya ya Kilombero akiwa na silaha ya kienyeji aina ya gobole risasi saba pamoja na vipande 20 vya nyama ya pori ya mnyama aina ya tohe.
Kamanda Mkama ameongeza kuwa katika operesheni hiyo silaha nyingine ya kienyeji aina ya gobole ilitelekezwa na wahalifu waliokuwa wakifuatiliwa na Polisi katika eneo la Chamwino Manispaa ya Morogoro huku juhudi za kuwakamata wahusika zikiendelea.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime