Athari zinazochangiwa na kutozingatia usafi unapoenda haja kubwa
WANAWAKE wengi hukumbwa na maambukizi hasa katika sehemu nyeti, baadhi yakichangiwa na desturi za kutozingatia usafi.
Matumizi ya choo na jinsi ya kuhakikisha usafi baada ya kumaliza haja kubwa au ndogo, ni mambo yanayofaa kuzingatiwa.
Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI): Bakteria kutoka kwenye haja kubwa, hasa E. coli, zaweza kusafiri hadi kwenye tundu la mkojo (urethra) na kusababisha maambukizi.
Hii ni mojawapo ya sababu kuu za maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI) kwa wanawake, kwani sehemu hiyo ya kutoa haja ndogo ni fupi na bakteria husafiri haraka.
Maambukizi ya uke
Bakteria au kinyesi kinapogusa uke hupunguza uwiano wa bakteria wazuri na kusababisha uke kutoa harufu, kutokwa na uchafu usio wa kawaida, kuwashwa au kuathiriwa na bakteria.
Mwasho wa ngozi
Mabaki ya kinyesi yanaweza kusababisha upele au mwasho mkali kwenye ngozi ya sehemu za siri.
Hatari ya maambukizi ya fangasi: Uke unapokuwa na unyevunyevu au uchafu, fangasi kama vile candida huongezeka kwa urahisi na kusababisha mwasho,uchafu mweupe mzito, harufu mbaya na maumivu.
Harufu mbaya kwenye sehemu za siri: Mabaki ya kinyesi yanayobaki bila kuondolewa husababisha harufu mbaya inayoweza kusumbua na kusababisha aibu.
Hatari ya maambukizi sugu: Ikiwa kutojipangusa vizuri ni tabia ya mara kwa mara, maambukizi ya UTI na uke yanaweza kurudia rudia, na wakati mwingine kusambaa zaidi hadi kwenye figo.
Jinsi ya kujiepusha na matatizo haya
Jipanguse kutoka mbele kuelekea nyuma: Kila mara tumia mtindo huo ili kuzuia bakteria kusogea kutoka sehemu ya haja kubwa kuelekea uke.
Tumia karatasi laini na safi: Epuka karatasi ngumu ambayo inaweza kusababisha michubuko kwenye ngozi.
Safisha kwa maji unapoweza: Kuoga au kusafisha sehemu hii kwa maji baada ya haja ni salama zaidi kuliko kupangusa bila maji.
Hakikisha sehemu hii inakauka kwani unyevu huzidisha fangasi na bakteria.
Vaa nguo za ndani za pamba: Pamba huruhusu hewa na hivyo kupunguza joto na unyevunyevu.
Epuka sabuni kali ukeni: Maji pekee yanatosha. Sabuni kali huharibu uwiano wa bakteria wazuri.
Muone daktari ikiwa una dalili kama vile maumivu unakojoa, harufu kali isiyo ya kawaida, kutokwa na uchafu usio wa kawaida, kuwashwa kwa siku nyingi, na maumivu ya chini ya tumbo
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii