Panya wasio na manyoya wavunja rekodi ya uzee- utafiti

Ni viumbe wa ajabu, wenye upara, wanaishi chini ya ardhi wakiwa na mwonekano unaofananishwa na soseji yenye meno, na sasa wataalamu wamefichua siri ya kijenetiki kuhusu siri ya wanyama hao kuishi maisha marefu.

Utafiti mpya unaonyesha kuwa wanyama hao wana utaratibu wa kurekebisha DNA ambao unaweza kuendeleza maisha yao kwa muda mrefu.
Panya hawa wanaoishi kwenye mashimo wanaweza kuishi hadi karibu miaka 40, na kuwafanya kuwa panya walioishi kwa muda mrefu zaidi duniani.

Matokeo mapya, yaliyochapishwa katika jarida la Sayansi, yanaweza pia kutoa mwanga kwa nini panya wasio na manyoya hustahimili magonjwa mengi yanayohusiana na umri.



Wanyama hao hawapatwi na saratani, uharibifu wa ubongo na uti wa mgongo, wala ugonjwa wa baridi ya viungo (arthritis), na kwa sababu hiyo, wanasayansi wengi wanataka kufahamu miili yao inavyofanya kazi.

Kwa utafiti huu, ulioongozwa na timu katika Chuo Kikuu cha Tonji huko Shanghai, Uchina, lengo lilikuwa uchunguzi wa vinasaba ,mchakato wa asili katika seli za miili.

Utafiti huu ulililenga kwenye protini fulani ambayo inahusika katika mfumo huo wa kutambua uharibifu na urekebishaji wa kijenetiki.
Seli inapohisi uharibifu, mojawapo ya dutu inayozalisha ni protini inayoitwa c-GAS. Hiyo ina majukumu kadhaa, lakini kilichowavutia wanasayansi hawa ni kwamba kwa binadamu, huingiliana na kudhoofisha mchakato ambao DNA huungana tena.

Wanasayansi wanafikiri kwamba kuingiliwa huku kunaweza kukuza saratani na kufupisha maisha ya binadamu.
Katika wasio na manyonya, watafiti waligundua kuwa protini hiyo huwa tofauti. Husaidia mwili kurekebisha chembe za DNA na kuweka jeniasili katika kila seli.

Profesa Gabriel Balmus ambaye anajishughulisha na masomo ya urekebishaji wa DNA na uzee katika Chuo Kikuu cha Cambridge, alisema kuwa ugunduzi huo ni wa kusisimua na ni "kielelezo cha mwanzo tu" cha kuelewa kwa nini wanyama hawa wanaishi maisha marefu isivyo kawaida.

Katika mamilioni ya miaka ya mabadiliko ya viumbe , Prof. Balmus alieleza kwamba aina hiyo ya panya wasio na manyoya huonekana kama wamebadilisha mfumo huo wa kijeni na kuutumia kwa manufaa yao.

"Ugunduzi huu unazua maswali ya kimsingi: jinsi mabadiliko haya yalivyosababisha protini sawa kutofautiana?
Ni nini kilibadilika? Na je, hii ni kesi pekee au sehemu ya muundo mpana wa mabadiliko?"

Muhimu zaidi, wanasayansi wanataka kujua ni funzo gani wanaweza kupata kutoka kwa panya hawa ili kuboresha afya ya binadamu na kupanua ubora wa maisha kulingana na umri.
"Nadhani kama tunaweza kubadilisha mfumo wa kibaiolojia wa panya wasio na manyoya," alisema Prof Balmus, "tunaweza kuleta matibabu yanayohitajika sana kwa jamii inayozeeka."

#Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii