Homa ya mapafu: 'Muuaji' mkubwa wa watoto duniani

Homa ya mapafu ni miongoni mwa magonjwa ambukizi yanaongoza kwa kusabisha vifo vingi miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Mary Wanjiku Murimi, mama wa watoto wanne, anaishi kusimulia jinsi mwanawe aliathirika na ugonjwa huu baada ya kuugua zaidi ya mara mbili.

Anatuelezea kuwa mwanawe wa pili alianza kupumua haraka huku akitoa sauti isio ya kawaida, akaanza kuwa mdhaifu, rangi yake kubadilika na kuhisi uchungu hali iliowalazimu kumpeleka hospitalini kwa ukaguzi wa kimatibabu.

'Tulipomfikisha hospitalini mara moja aliwekewa hewa ya oksijeni kwani hali yake ilisimekana kuwa mbaya, akafanyiwa vipimo vilivyobaini yuko na homa ya mapafu na kulazwa hospitalini kwa siku kadhaa', alisema Mary.

Kupatikana kwa mwanawe na maradhi hayo kulimshtua sana kwani anajua madhara yake na ameshuhudia watoto wengi wakifariki

' Tulianza kujiuliza alipata ugonjwa huu lini na aliutoa wapi kwasababu haukuwa msimu wa baridi, ilikuwa hali ya kushutua kumwona mwanangu amewekwa kwenye mashine ya oksijeni huku akiwa na maumivu mengi'

Kulingana na Dkt Margaret Wainaina - daktari wa watoto na aliye na uzoefu wa kutibu magonjwa ya kifua anaelezea kuwa homa ya mapafu husababishwa na viini tofauti kama virusi, bakteria au kuvu (fungi) pamoja na kukosa hewa safi.


Je, homa hii ni aina ya maradhi gani?
Homa ya mapafu ni ugonjwa unaoathiri mapafu ya mtu. Mapafu ya mtu kwa kawaida huwa na mifuko midogo inayojulikana kama 'alveoli' ambayo kwa kawaida huwa yamejaa hewa wakati mtu mwenye afya anapopumua.
Mtu anapoathirika na ugonjwa wa homa ya mapafu mifuko hiyo ya alveoli hujaa maji na kufanya kupumua kuwa vigumu na uchungu kudhibiti kiwango cha hewa ya oksejeni anayopumua.

Dalili za maradhi haya
Dalili za ugonjwa huu wa mapafu miongoni mwa watoto ni kama vile joto jingi mwilini, kupumua kwa haraka, kukohoa, maumivu kifuani, kutoa sauti iso ya kawaida wakati wa kupumua, mtoto kupata ugumu wa kula au kunyonya, na wakati mwingine kuzimia.
Dkt Wainaina anaelezea kuwa homa ya kawaida huja na makamasi, kufungana kwa sehemu zote zinazohusika na kupumua ila homa ya mapafu humfanya mtu kupumua kwa haraka kuliko kawaida na pia mtoto hukosa kuwa mchangamfu.

Watoto wachanga ndio wapo katika hatari kubwa ya kuambikizwa ugonjwa huu ila pia watu wazima huambukizwa homa hii hatari.
Baada ya kupitia masaibu hayo, Mary sasa amekuwa makini na mwanawe na akianza kuonyesha dalili zozote za awali, wao humfikisha hospitalini mapema bila kuchelewa
' Wazazi wanafaa kujua si kila kikohozi ni homa ya kawaida, na wazazi wasizoee kupuuza, ni vyema ufike hospitalini na mwanao, uambiwe na dakatri kama ni homa ya kawaida au homa ya mapafu kuliko kumtibu mwanao mwenyewe bila uhakika' anasema Mary

Takwimu zinasemaje kuhusu homa ya mapafu?
Kwa mujibu wa takwimu za maradhi hayo kote duniani, mtoto mmoja hufariki kutokana na ugonjwa huo kila baada ya sekunde 43 huku watoto 84 wakifariki kila saa . Vilevile WHO imethibitishwa kwamba watoto zaidi ya elfu mbili hufariki kila siku huku 735,840 wakifariki kila mwaka wakiwemo watoto wachanga 200,000.
Hii ni kulingana na ripoti ya shirka la Afya duniani (WHO) kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu.
Ugonjwa huu pia husabisha asilimia kumi na tano ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Aidha visa 1,400 kote duniani huripotiwa miongoni mwa watoto laki moja ambao hufikishwa hospitalini.

Maeneo yalioathirika pakubwa..
Eneo la bara Asia ndilo linaongoza katika visa vingi vya homa ya mapafu, likifuatwa na mataifa ya Afrika Magharibi na Afrika ya kati.
Nchini Kenya, homa ya mapafu bado ndiyo inayoongoza katika kusababisha vifo miongoni mwa watoto walionchini ya umri wa miaka mitano.
Kulingana na ripoti ya UNICEF mwaka wa 2019, asilimia kumi na nne ya vifo vya watoto vilitokana na homa ya mapafu, huku Kenya ikishikilia nafasi ya 28 katika mataifa barani Afrika yenye idadi ya juu ya vifo vya watoto kutokana na Homa ya mapafu.

Kulingana na ripoti hiyo ya Unicef, vifo vingi vya homa ya mapafu miongoni mwa watoto hutokana na umaskini ambao husababisha lishe duni, ukosefu wa maji safi ya kunywa, hali mbaya ya hewa ndani ya nyumba na nje pia, na kutopata huduma stahiki ya afya.


Chanjo
Chanjo ya homa ya mapafu inasemekana kuwa muhimu katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.
Ugonjwa huu hutibiwa vyema iwapo utagunduliwa mapema.
Kulingana na Dkt. Wainana ugonjwa huu una matibabu tofauti kulingana na chanzo chake, huku akionya matumizi ya dawa aina ya antibiotic bila ushauri wa daktari .

Maambukizi
Njia moja ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu hatari miongoni mwa watoto, ni kuhakikisha mtoto anapokea chanjo zote zinazohitajika ikiwemo chanjo ya homa ya mapafu, kuhakikisha kuna hewa safi majumbani, usafi unadumishwa wanapokaa na kucheza na pia kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama miezi sita za kwanza ili kuimarisha kinga yao ya mwilini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii