Mkuu wa Chuo cha Taaluma Ya Polisi Dar es Salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dkt. Lazoro B. Mambosasa, amewataka maofisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kufanya kazi kwa weledi na uadilifu baada ya kumaliza mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wakufunzi wa Chuo hicho.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo leo Oktoba 22 mwaka huu Dkt. Mambosasa amesema mafunzo hayo yatasaidia katika kuimarisha utendaji kazi na kuwajengea uwezo ujuzi na weledi kwa kozi zijazo za kitaaluma na za uongozi.
Aidha Dkt. Mambosasa amewapongeza wawezeshaji kutoka ndani ya Chuo hicho kwa kuonesha taaluma ya kiwango cha juu katika ufundishaji na utoaji wa mafunzo hayo pia amewakumbusha wakufunzi kuhusu kusimamia mafunzo na kuwarithisha wale ambao kwa namna moja au nyingine hawajafanikiwa kuyapata.
Naye Mkuu wa Mafunzo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrea Legembo amewataka wakufunzi hao kutumia nyenzo na mbinu mbalimbali walizozipata kwenye mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo kwa muda mfupi kwani changamoto nyingi zimetatuliwa kupitia mafunzo hayo na matarajio ya chuo kuona wateja wa ndani na nje wananufaika
Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo askari yalijumuisha jumla ya wakufunzi 46 na yalianza rasmi Oktoba 15 mwaka huu na kuhitimishwa Oktoba 22 mwaka huu.