KATIKA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu sekta ya habari nchini imeelekezwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani ya nchi, kuhakikisha taarifa sahihi, na kudumisha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Viongozi wa serikali, wataalamu wa habari na wasimamizi wa sheria wamekutana na kutoa maelekezo mahususi yanayolenga kuiweka tasnia ya habari katika mstari wa uwajibikaji wa kitaifa.
Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, anatoa mwito kwa waandishi wa habari kuhakikisha wanatumia taaluma yao kulinda mshikamano wa taifa.
Anasema katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi, taarifa nyingi husambaa na baadhi huweza kuvuruga amani, ikiwa hazitachakatwa kwa weledi.
“Zingatieni weledi wa taaluma yenu kwa kufuata maadili ya uandishi wa habari. Pili, msimame imara kama walinzi wa amani na mshikamano wa kitaifa. Tatu, lindeni heshima ya tasnia yenu dhidi ya uzushi, uchochezi na taarifa zisizothibitishwa,” anasema Dk Biteko.
Anaeleza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kutumia lugha ya staha na kuepuka upendeleo, hasa wakati wa kampeni na kuripoti matokeo ya uchaguzi.
“Sekta ya habari ni nyenzo muhimu sana kulinda na kudumisha amani katika kipindi chote cha uchaguzi,” anasema na kusisitiza kwamba, taarifa zenye taharuki zinaweza kuigawa jamii na kuathiri mshikamano wa taifa.
Katika mkutano huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi anasema sekta ya habari imebeba dhamana ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, usawa na kwa uelewa wa kutosha kwa wananchi.
Anasisitiza kuwa, katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii, kumekuwa na changamoto ya upotoshaji wa taarifa, lugha za chuki, na habari zisizo na uthibitisho. “Ni dhahiri kuwa sekta ya habari inabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha mchakato huu unafanyika kwa amani, usawa na kwa uelewa wa kutosha kwa wananchi,” anasema Profesa Kabudi.
Anasema wizara yake inafanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari na kuweka mazingira bora ya kazi kwa wanahabari. Anafafanua kuwa zaidi ya waandishi 2,900 wamesajiliwa kupitia mfumo wa ‘Tai Habari’ na kupatiwa vitambulisho vya kidijiti na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanaofanya kazi za habari ni waliothibitishwa kisheria.
Akiwasilisha taarifa ya msingi kuhusu wajibu wa sekta ya habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JAB, Patrick Kipangula anasema sekta hiyo inasimamiwa na Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ambayo, kupitia kifungu cha 11, naunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.
Anasema bodi hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusajili na kutoa ithibati kwa wanahabari, kulinda maadili ya taaluma, kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili na kuchukua hatua za kinidhamu inapobidi. Kwa mujibu wa Kipangula, Kifungu cha 19 cha sheria hiyo kinakataza mtu yeyote kufanya kazi za kihabari bila ithibati ya bodi, hasa katika kipindi nyeti kama uchaguzi.
Anasema wanahabari wana wajibu wa kutoa taarifa sahihi kabla, wakati na baada ya uchaguzi ili kusaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi. “Katika kipindi cha uchaguzi,” anasema, “Waandishi wa habari wana wajibu wa kutoa elimu kwa wapiga kura kuhusu haki zao na namna ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.”
Aidha, anasema wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu wagombea, sera zao na mipango yao, hivyo kuwasaidia wapigakura kufanya uamuzi wenye uelewa sahihi na wa kutosha. “Baada ya uchaguzi, wanapaswa kuripoti matokeo, kuchambua mchakato wa uchaguzi na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi waliowekwa madarakani,” anasema.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Mkuu wa Huduma za Utangazaji, Andrew Kisaka inatoa tahadhari kwa vyombo vya habari juu ya kuripoti migogoro na maafa wakati wa uchaguzi. Kwa mujibu wa Kisaka, wakati wa uchaguzi kuna mazingira ya mgawanyiko wa kijamii, mivutano na upotoshaji wa hali ya juu.
Kwa msingi huo Kisaka anasema ni muhimu kuepuka kusambaza taarifa za uongo au kuchochea migogoro. Anasisitiza kwamba si kila tukio linapaswa kuripotiwa hasa yale yanayohusiana na watu wenye ushawishi wanaotoa kauli za chuki.
Anahimiza matangazo ya moja kwa moja ya machafuko au mikusanyiko yenye mvutano yafanyike kwa umakini mkubwa na yaendeshwe na waandishi waandamizi waliopatiwa mafunzo maalumu. “Lugha ya uchochezi inaweza kuwa habari, lakini usirudie maneno hayo kwenye kichwa cha habari. Tafuta kauli za kulaani vurugu kutoka kwa upande huo huo,” anafafanua.
Katika muktadha huo huo, Dk Egbert Mkoko kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anatoa mwongozo kwa vyombo vya habari kuhusu namna ya kuripoti Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa uadilifu.
Anasema kila chombo cha habari kinapaswa kuchapisha taarifa sahihi, zinazoweza kuthibitishwa na zilizohakikiwa na kuepuka kubashiri, kueneza uvumi au kupendelea upande wowote. Dk Mkoko anahimiza wanahabari kutoripoti madai yasiyothibitishwa au yenye nia ovu kupitia teknolojia ya kidijiti.
Anasema vyombo hivyo vinapaswa kuepuka maudhui yanayoleta chuki, ubaguzi au kuchochea vurugu. Anavitaka kuweka uwiano wa taarifa kwa vyama vyote vya siasa na wagombea wao, kufanya matangazo yanayolipiwa yatambuliwe wazi kama matangazo na yasichanganywe na habari.
Anahimiza waandishi wote walioko kazini kuhakikisha katika kipindi cha uchaguzi wanakuwa na ithibati kutoka JAB. “Pia wanapaswa kuripoti vitisho, mashambulizi au vizuizi dhidi ya waandishi kwa vyombo husika, zikiwemo Polisi na Idara ya Habari-MAELEZO,” anasema.
Aidha, Dk Mkoko anakumbusha kuwa waandishi hawapaswi kushiriki kampeni au shughuli za vyama vya siasa ili kuepuka mgongano wa maslahi. “Lugha ya kuripoti iwe ya Kiswahili au Kiingereza, isipokuwa panapohitajika Mkalimani,” anasema.
Kwa upande wake, Humphrey Mtui kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) anasisitiza umuhimu wa kulinda taarifa binafsi katika muktadha wa uchaguzi.
Anasema Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022 inalenga kuhakikisha taarifa kama vile rejesta za wapigakura, taarifa za vyama, namba za vitambulisho na taarifa za kibayometriki zinakusanywa na kuchakatwa kwa mujibu wa sheria.
Mtui anasema vihatarishi kama upatikanaji usioidhinishwa wa taarifa, matumizi ya taarifa kwa nia ya kisiasa, uvujaji wa data au kukusanya taarifa bila ridhaa sahihi vinaweza kuathiri imani ya wapigakura na uhalali wa uchaguzi.
Katika mapendekezo yake, PDPC inahimiza taasisi husika kushirikiana, kutoa elimu ya haki za faragha kwa wapigakura, kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuhakikisha vyama vya siasa vinawajibika katika usalama wa taarifa wanazokusanya.
“Kwa mujibu wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Tanzania inayowajibika kidijiti, ulinzi wa taarifa binafsi ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki. Kulinda taarifa binafsi ni kulinda demokrasia,” anasema.
Kwa ujumla, wadau wote wamesisitiza vyombo vya habari na wanahabari kuwa wananafasi ya kipekee kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 unafanyika kwa misingi ya ukweli, haki, usawa na utulivu.