Vita ya hoja na vijembe imeendelea kupigwa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kila upande ukiutuhumu mwingine kwa mwenendo usiofaa.
Chadema inautuhumu uongozi wa Chaumma kujaa usaliti kwa kuwa wengi wao walikuwa makada wa chama hicho kikuu cha upinzani lakini wamekihama katika nyakati ngumu bila kujali walisaidiwaje kabla.
Kwa upande wa Chaumma kinajibu mapigo dhidi ya Chadema kikiwatuhumu baadhi ya viongozi wake wa juu kwa tabia ya kutweza utu wa wanawake katika majukwaa ya kisiasa huku kikiwataka watoke hadharani kuomba radhi.
Licha ya vijembe baina yao vyama hivyo vilivyopo ziarani katika mikoa tofauti Chadema ikiwa Dodoma na Chaumma ikiwa Geita vyote vina uwiano wa hoja kuhusu rasilimali za nchi vikisema wingi wake hauakisi uchumi wa Taifa.
Katikati yao kinapita Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoendelea na ziara yake mkoani Arusha chenyewe kikisimama kati kuwataka wananchi wawakatae viongozi wanaopandikiza chuki kwa kutumia dini.
Hayo yote yamejiri jana Jumapili 2025 katika ziara za viongozi wa vyama hivyo vitatu CCM Chadema na Chaumma katika mikoa ya Arusha Dodoma na Geita ikiwa ni mwendelezo wa maandalizi ya kuuza sera kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu. Ingawa Chadema hakitashiriki uchaguzi huo kikidai kuwapo kwa mabadiliko kwanza.
Chadema na Chaumma vijembe Katika ziara ya No reforms no election mkoani Dodoma Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara John Heche ametupa kijembe kwa waliokihama chama hicho akisema hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa mbunge.
Licha ya kauli hiyo ya Heche kati ya waliokihama chama hicho yupo Suzan Kiwanga aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum na baadaye wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro kadhalika Devotha Minja aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.