Takukuru Mtwara kuwanufaisha wakulima wa korosho kutoka kwa vyama vya msingi

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara imefanikiwa kusaidia wakulima kulipwa kiasi cha shilingi milioni 79.8 ambazo walikuwa walikuwa wakizidai kutoka kwenye baadhi ya Vyama vya Msingi na Ushirika (AMCOS) kufuatia elimu na uhamasishaji unaoendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara Bw. Mashauri alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi waliotoa taarifa kuhusu ubadhirifu wa fedha za wakulima katika baadhi ya vyama hivyo vya ushirika baada ya kufanya uchunguzi wa kina fedha hizo zilirudishwa kwa wakulima.

Aidha Bw. Mashauri alibainisha kuwa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imefungua jumla ya majalada saba ya uchunguzi kuhusiana na tuhuma mbalimbali za rushwa na kwamba uchunguzi wa majalada hayo uko katika hatua mbalimbali.

Katika kipindi husika jumla ya malalamiko 82 yalipokelewa na TAKUKURU ambapo malalamiko 44 yalihusiana na rushwa na 38 hayakuhusu rushwa Malalamiko ya rushwa yamegawanyika katika sekta mbalimbali zikiwemo: Ushirika (16), Afya (14), Maendeleo ya Jamii (9), Utawala (1), Ardhi (1), Kilimo (1), Elimu (1), na masuala binafsi (1).

Hata hivyo TAKUKURU bado inaendelea kuhimiza wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa pindi wanaposhuhudia vitendo vya rushwa katika maeneo yao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii