Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesema ni muhimu kufanya mazoezi ili kuwa na misuli imara uzeeni.
Profesa Janabi alisema hayo alipozungumza katika kipindi cha Busati la Mtoro kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ZBC2 cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Alisema ni muhimu watu waweke akiba ya afya kwa kufanya mazoezi na kula vyakula vinavyojenga afya.
“Watu wazima miaka 70 au 80 hawawezi kutembea si kwa sababu ya umri ni kwa sababu hawana misuli, misuli imeisha nguvu kwa sababu katika ujana wake alikuwa hafanyi mazoezi,” alisema Profesa Janabi.
Aliongeza: “Ukienda Japani, mzee ana miaka 85 anakwenda sokoni, anapanda basi mwenyewe, wale akiba waliyoweka ni kipindi hiki na hakuna aliyechelewa kufanya mazoezi, tembea, nyanyua vyuma kidogo vya kawaida… kwa hiyo mbali ya kuweka akiba ya fedha tuweke akiba ya afya.”
Profesa Janabi alieleza umuhimu wa kula mbogamboga na matunda, kunywa maji mengi hasa kwa wakati huu wa mfungo wa Ramadhani ili kuwezesha mwili kuwa na maji.
“Tunapokuambia kula mboga za majani si kwa ajili yako ni kwa ajili ya kuwalisha wale wadudu kwa sababu kadri wanavyokuwa wengi ndio wanavyokupa wewe kinga yako… tunasisitiza sana usinywe juisi kula matunda, nawashauri kula matunda matunda yote yana sukari hakuna tunda lisilo na sukari.”
Pamoja na hayo Profesa Janabi alieleza dalili za ndani za ugonjwa wa saratani ya tezi dume.
“Dalili za mwanzo kabisa, unakwenda haja ndogo lakini unaona bado kuna haja imebaki unakwenda msalani unatoa haja ndogo kidogo tu unaona umemaliza kwa sababu lile tezi kadri linavyokua kubwa linabana ule mrija wa haja ndogo,” alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa “Hatari yake kubwa ni kuwa saratani ya tezi dume haina haraka, inakaa na wewe miaka 15, 20 bahati mbaya wengi tunaokuja kuwaona inakuwa ishatoka kwenye sehemu za siri imesambaa”.
Profesa Janabi aligusia kuhusu uhusiano wa kukoma kwa hedhi na kuongezeka kwa uzito na vitambi kwa wanawake akisema ni kutokana na mabadiliko ya mwili yanayosababishwa waonekane wamebadilika.
“Sio kama amebadilika, ni mwili unafanya anakuwa na hasira sana, hawezi kulala, anasikia joto sana, na tiba zipo kwenye hospitali zetu mlete mama apate ushauri na kama anahitaji homoni ni vidonge tu kuweza kurudisha,” alisema.
Alisema hicho ni kipindi ambacho mafuta yaliyokuwa kwenye mapaja yanakwenda kwenye tumbo.
“Ndio pale unamuona mama ana kitambi, anakuwa hali sana lakini anakuwa na kitambi,” alisema.