Sababu ya watu maskini kuzongwa na maradhi ya kisukari na shinikizo la damu

WAKENYA 372,000 wa tabaka la wenye mapato ya chini wamebainika kuugua maradhi ya kisukari na shinikizo la damu ndani ya miezi minne iliyopita, asasi za afya zimefichua.


Kati ya hawa, wagonjwa 106, 000 wameagizwa kufanyiwa ukaguzi wa kina kuhusu kisukari baada ya watu 5.51 milioni kupimwa kote nchini.


Watu wengine 272, 000 walipatikana na ugonjwa wa shinikizo la damu baada ya jumla ya watu 3, 89 milioni kupimwa.


Hii ni kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa mfumo wa habari za kieletroniki kuhusu afya ya jamii (eCHIS) unaotuma data kuhusu ukaguzi wa magonjwa moja kwa moja kutoka kwa watu wanaotembelewa na wahudumu wa afya ya kijamii (CHPs).


Wahudumu wa CHPs hutumwa katika maeneo ya mashinani, haswa wanakoishi watu wenye mapato ya chini kuwafanyia ukaguzi wa kiafya.


Watu kama hao huishi katika mitaa ya mabanda, na vijijini.


Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ugonjwa wa kisukari hudhihirika kutokana na kupanda kwa viwango vya sukari kwenye damu.


Baada ya muda, hali hii husababisha kuharibika kwa moyo, mishipa ya damu, macho, figo na mishipa ya hisia.


Data ya hivi punde kutoka kwa Wizara ya Afya inaonyesha kuwa jumla ya Wakenya 266, 000 waliagizwa kufika katika vituo vya afya kote nchini kufanyiwa ukaguzi zaidi.


Hii ni baada ya watu 3, 890,000 kufanyiwa ukaguzi kubaini ikiwa wanaugua maradhi ya shinikizo la damu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii