Wengi ambao wametinga ukongwe huwa na tatizo la misuli yao kuisha nguvu au kulegea, ugonjwa ambao unafahamika kwa kimombo kama ‘Sarcopenia’.
Ugonjwa huo hulemaza uwezo wa mwanaume kuwajibikia majukumu ya kawaida hata kazi nyumbani baada ya kutinga uzee (wale ambao wana umri wa miaka 60 na zaidi) kwa sababu misuli yao huisha nguvu.
Kati ya mambo ya kawaida ambayo mtu hawezi kufanya akiwa na ugonjwa huo ni kutaabika akitembea, hawezi kupanda vidato au ngazi, kuanguka mara kwa mara huku misuli ikidhoofika kabisa.
Japo kisababishi kikuu cha maradhi hayo ni uzee, kukosa kufanya mazoezi mara kwa mara, uzani kupita kiasi, kupungua kwa homoni mwilini na kisukari pia huchangia misuli kulegea au kudhoofika kiasi cha mtu kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, Wanasayansi sasa wamebaini kuwa kafeni ambayo ipo kwenye kahawa inasaidia sana katika kujenga misuli imara au kuimarisha ile inayoelekea kudhoofika.
Kafeni inazuia kutanuka kwa seli za mwili na pia hulemaza chembechembe za sumu ndani ya mwili hasa ile inayofifisha utendakazi wa misuli.
“Utafiti huu unaonyesha kuwa unywaji wa kahawa au kafeni unahusishwa na misuli kuwa imara. Unaonyesha kuwa unywaji wa kahawa na kupata kafeni ni mbinu ya kuzuia kupotea au kupungua kwa misuli miongoni mwa wanaume,” ukasema utafiti huo uliofanywa China.