Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar kwa lengo la kuendeleza ushirikiano na Uingereza katika kuwezesha na kukuza Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Uingereza.
Akiongea
na Balozi wa Uingereza Ofisi za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na
Biashara Mtumba, Dodoma, Waziri Kijaji amesema Tanzania itaendelea
kushirikiana na Uingereza kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Serikali kwa
Serikali (G2G) kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza yalioyolenga
kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na
Uingereza.
Naye,
Balozi Concar amesema kuwa Serikali ya Uingereza itaendelea kutekeleza
maazimio hayo kwa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mpango kazi
jumuishi unaolenga kuziwezesha taasisi za umma na binafsi zinazohusika
na Uwekezaji na Biashara kupanga vipaumbele vya kibiashara
vinavyotekelezeka kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali yanayoweza
kujitokeza.
Kongamano
la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lilifanyika
Novemba 16, 2021, Dar es salaam na lililenga kupanua zaidi wigo wa
ushirikiano katika maeneo ya biashara na uwekezaji hususan sekta za
nishati, madini, miundombinu, kilimo, uchumi wa bluu na utalii,
kuhamasisha wafanyabiashara wa Uingereza kuja kuwekeza nchini na
wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao Uingereza.