WAKATI pacha wake James Mwema (aliomba jina libadilishwe) walikuwa wanazaliwa, ilikuwa siku njema maishani mwake.
Hata hivyo, walipofikisha umri wa miezi mitatu na nusu, pacha hao hawakuwa wanalala ipasavyo mchana na hata usiku.
“Walikuwa wanalala tu kwa dakika thelathini na iwapo mmoja wao angeamka na aanze kulia, mwenzake angefuata. Usiku vilevile, walikuwa wakiamka angalau mara kumi au kumi na mbili,” anakumbuka.
Kutolala kwa pacha hao, kuliathiri pia wanavyokula na hata hisia zao huku mara nyingi wakilia sana. Walipofikisha umri wa miezi mitano na nusu, Bw Mwema alitafuta usaidizi wa mtaalamu wa usingizi.
“Tuligundua kuwa kila mtoto alikuwa na tabia na hisia zake za kipekee (different personality) na nyakati tofauti za kulala. Kwa hivyo tukatengeneza ratiba ya kila mmoja wao, nyakati za kuwapa chakula na kuwabadilisha nepi.”
Kwa kufuata maagizo waliyopewa na mkewe, Bw Mwema aligundua kuwa mmoja wa pacha wake alikuwa akihisi usingizi saa kumi jioni na mwenzake saa kumi na mbili.
“Tuligawanya vyumba vyao vya kulala kiasi kwamba iwapo mmoja wao angeamka asingeamsha mwenzake. Pia, tulihakikisha kuwa wanapolala mchana, hawalali kwa zaidi ya saa mbili,” anaeleza.
Hata hivyo, watoto hao walipoendelea kukua ratiba zao zilibadilishwa tena lakini si sana.
“Ili tusiingilie kati usingizi wao kila wageni walipotutembelea, hatuwaamsha mpaka wao wenyewe waamke. Kutowaamsha kuliwasaidia kupata usingizi wa kutosha na hivyo hawakusumbua baadaye.”
Mwende Kimweli, mtalaamu wa usingizi anasema kuwa mtoto mchanga hadi afikishe miaka mitatu anapaswa kulala kwa dakika 45 hadi saa mbili mchana na kati ya saa kumi na kumi na moja kila usiku.
“Asipolala vyema usiku, mtoto huyo hatalala vizuri mchana. Atalala baada ya saa sita usiku, aamke sana katikati ya usiku kisha ataamka mapema sana asubuhi. Aidha, hulia sana na kuonekana kukerwa sana (cranky),” anafafanua.
Kutorekebisha hali hii, Bi Kimweli anasema huathiri pia ukuaji wao haswa wanapofikia umri wa kuenda shule.
“Utapata mtoto huyu anatatizika kuelewa kinachofunzwa shuleni, anategwa au kuanguka sana, atashindwa kuamka kuenda shuleni, hatakula vizuri, hulia sana na huwa mwenye uchovu mwingi.”
Kutokuwa na ratiba ya wakati mtoto anapaswa kulala mchana na kwa saa ngapi huathiri muda atakapolala usiku. Isitoshe, Bi Kimweli anaeleza kuwa ratiba hii inapaswa kutilia maanani ukuaji wa mtoto kama anavyoanza kutembea, kuongea, na hata kuelewa mazingira yake.
Licha ya kwamba siku za kwanza za kufuatilia ratiba hii zitakuwa ngumu, Bi Kimweli anaeleza kuwa ni muhimu kuwaelimisha wanafamilia wote anaoishi nao mtu kuhusu mabadiliko hayo.
“Mtoto aliapo sana unapomweka chini alale, huenda ikawa mtoto huyo alikuwa amechoka sana kutokana na yale amefanya mchana au ule uchovu wa miezi kadhaa au miaka ya kutolala vizuri,” anaeleza.
Japo nyakati ambapo watu hulala hutofautiana kutoka nyumba moja hadi nyingine, Bi Kimweli anasema kuelewa ratiba ya mzazi pia kunasaidia kutengeneza ratiba ya mtoto.
Wakati mwingine, wazazi wengi hupendelea kuwalaza watoto wao kwenye vitanda vyao kwanza, kisha kuwahurumia na kuwarudisha kitandani pao wanapoanza kulialia. Hata hivyo, Bi Kimweli anashauri kwamba ni bora kuhakikisha mtoto analala katika kitanda chake mwenyewe pindi tu anapoanza kusinzia.
“Tabia ya wanandoa kulala na mtoto kwenye kitanda chao huathiri pia usingizi wa mtoto kwani huenda akahisi joto jingi au akawa hatulii mnapogeuka geuka kwenye kitanda na hivyo basi mtoto akashindwa kulala vyema,” anashauri.
Dalili za kujua iwapo mtoto wako anahisi usingizi kama anavyoeleza Bi Kimweli ni anapoanza kulia, kusugua macho yake, kuvuta nywele zake, na kuangalia kitu kwa muda mrefu.
“Watoto wakubwa kiasi huanza kujigeuza geuza kwenye sakafu, kutaka kushikwa au kuwa karibu na mzazi wake au hata wanapokuletea blanketi.”
Huku dunia ikiadhimisha Siku ya Usingizi Ijumaa wiki jana, lengo kuu likiwa kuangazia tofauti za usingizi mwema kwa watu duniani na athari zake kwa afya, wanasayansi walisisitiza kuwa ukosefu wa usingizi wa kutosha unaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya mwili na akili.
Usingizi wa kutosha ni muhimu kwa kazi mbalimbali za mwili, ikiwa ni pamoja na mfumo wa kingamwili (immune system), mabadiliko ya chakula mwilini kimetaboliki, udhibiti wa homoni na afya ya moyo.
Kwa upande mwingine, kutopata usingizi wa kutosha kumehusishwa na hatari kubwa ya magonjwa ya muda mrefu kama vile kuwa na uzito uliopindukia (obesity), kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.
Bi Kimweli anasema, “Kila mtu mkubwa kwa mdogo anafaa kuwa makini na saa anazotumia kulala kila siku. Iwapo una matatizo ya kulala, tafuta ushauri wa mtalaamu.”