NI jukumu la mzazi kusaidia watoto wake kutumia dijitali kukuza talanta zao.
Kulingana na mtaalamu wa malezi dijitali , wazazi wanaweza kutumia teknolojia ya dijitali kukuza vipawa vya watoto wao huku wakihakikisha usalama wao.
“Teknolojia ya dijitali ina majukwaa ambayo mzazi anaweza kutumia kukuza vipawa vya wanawe. Watoto wanaweza kuyatumia kuandika blogu au kujifunza michezo tofauti, muziki, kupiga picha na kuuza bidhaa. Wanaweza kunoa vipawa vyao katika mambo mengi. Kupitia dijitali, wanaweza kuuza kazi zao. Hivyo basi, wazazi wanapaswa kuwahimiza na kuwaongoza kuafikia kwa kuwa wabunifu,” asema mtaalamu wa malezi Vicky Simon.
Mtaalamu huyu anasema wazazi wanaoruhusu watoto wao kuanza kutalii ulimwengu wa dijitali kwa lengo la kukuza talanta zao, huwa wanawapa ufunguo wa ufanisi katika maisha yao ya siku zijazo.
Simon anasema wazazi wanastahili kuwasaidia watoto wao kuonyesha talanta zao kupitia mtandao ili kuwatia motisha.
“Kukumbatia mtandao ni njia moja ya mtoto wako kuweka rekodi ya ufanisi wake, iwe ni picha yao wakipokea zawadi, wakishiriki na kushinda mechi au wakiwa kwenye hafla muhimu kwa maisha yao. Hii inaweza kuwatia moyo kukuza talanta zinazoweza kuwafaa katika maisha yao ya baadaye,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema wazazi wanafaa kuchunguza na kuidhinisha kile watoto wao wanachapisha kwenye mtandao ili wasihatarishe maisha yao na ya familia zao.
“Ni muhimu kabisa kuwa makini ili watoto wasianike maelezo au kuchapisha chochote mtandaoni kinachotoa maelezo yanayoweza kutumiwa na wahalifu kuwadhuru kwa njia yoyote,” anaongeza.
Vitu vinavyoweza kuepukwa ni kama sare za shule, picha zinazotambua wanakoishi au kusomea chapisho lolote linalotangaza watakakokuwa.