HUKU idadi ya binadamu ikiendelea kuongezeka ulimwenguni na chakula kuwa haba, wanasayansi wamebaini kuwa kula wadudu ambao wana viwango vya juu vya protini kutakuwa jambo la kawaida miaka mingi inayokuja.
Jinsi idadi ya watu inavyoongezeka ulimwenguni ndivyo ardhi za kushiriki shughuli za kilimo na ufugaji zinazidi kudidimia. Mara nyingi binadamu hutegemea ulaji wa nyama kutoka kwa mifugo ili kupata madini ya protini.
Hata hivyo, kilimo kina gharama ya juu ikizingatiwa huhusisha matumizi ya maji mengi na huchangia kupanda kwa joto ulimwenguni.
Utafiti umeonyesha kuwa kilimo hutoa aina ya gesi ya kaboni ambayo ni asilimia 18, kiasi cha juu hata kuliko magari ya uchukuzi barabarani.
Kwa sasa idadi ya watu ulimwenguni ni zaidi ya bilioni saba japo Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) limesema idadi hiyo itapanda hadi zaidi ya watu bilioni 10.
Kutokana na mbinu za kusaka chakula kuendelea kuwa haba, watafiti wanasema kuwa kula wadudu kutakuwa njia bora ya kupata madini ya protini.
Kiasi cha gesi za kaboni, nitrojeni na methani kinachotokana na ufugaji wa wadudu kipo chini sana na hii inaonyesha kuwa ufugaji huo hauna athari kwenye mazingira.
Shirika la Chakula Duniani (FAO) linakadiria kuwa kufikia 2025, zaidi ya watu bilioni 1.8 watakuwa wakiishi maeneo ambayo yanakabiliwa na uhaba wa maji.
Hata hivyo, ufugaji wa wadudu unaweza kusaidia kwa sababu hauhitaji maji mengi na pia wadudu wanastahimili ukame mtupu.
“Kati ya manufaa makubwa ya ufugaji wa wadudu ni kuwa mahitaji ya maji ni madogo sana ikilinganishwa na ufugaji wa mifugo. Wadudu hata hupata maji kwa kula mimea freshi,” ukasema utafiti uliochapishwa kwenye tovuti ya Science Direct.
Utafiti uliochapishwa kwenye tovuti ya Molecular Diversity Preservation International (MDPI) uliweka wazi manufaa ya kula wadudu waliopikwa vizuri. Kuna aina 1,900 ya wadudu ambao wanaliwa ila dhana kuwa viumbe hao hawawezi kuwa kitoweo ndiyo imesababisha binadamu kukwepa ulaji wao.
“Wadudu wana protini ambayo ina asidi muhimu ya amino katika viwango bora kwa manufaa ya binadamu. Wengi wa wadudu ambao wanaliwa wana madini ya ayoni, zinki na aina ya vitamini E,” ukasema utafiti uliochapishwa na MDPI.
Kati ya wale ambao wanavumisha hoja ya wadudu kuliwa kama njia mbadala ya kupata proteni ni Dkt John Kinyuru, mhadhiri mkuu katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (Jkuat).
Dkt Kinyuru anasema Kenya ina aina 19 ya wadudu ambao wanaweza kuliwa ikiwemo mende, nzige, panzi, nzi wa nyumbani miongoni mwa wadudu wengine.
“Tunawafuga wadudu hawa. Kwa mfano nzi wa nyumbani wanaweza kufugwa kisha watumiwe kuwalisha nguruwe na samaki na hawa bado huliwa na binadamu,” akasema Dkt Kinyuru.