Abdullahi Mire, mkimbizi kutoka Somalia ameshinda tuzo ya wakimbizi ya UNHCR

Mire alizaliwa kusini mwa Somalia mwaka 1987 na aliishi katika kambi ya Dadaab nchini Kenya miaka ya 1990 wakati familia yake ilipotoroka kutoka Qoryooley katika mkoa wa Lower Shabelle kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia

Mkimbizi wa zamani mtoto kutoka Somalia, Abdullahi Mire ametajwa kuwa mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya wakimbizi ya UNHCR inayojulikana kama Nansen Refugee Award. Abdullahi Mire mwenye miaka 36 alitambuliwa kwa kuleta vitabu 100,000 kwa wenzake waliokuwa katika kambi mbai mbali nchini Kenya.

“Mwaka jana wa 2022, Angela Merkel, Chansela wa zamani wa Shirikisho la Ujerumani, alishinda tuzo na leo ni mkimbizi kijana kutoka Dadaab. Anga haina kikomo”, Mire aliiambia VOA Idhaa ya ki-Somali.

Akizungumza kabla ya kutangazwa kwa tuzo hiyo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi, Filippo Grandi amempa heshima Mire kwa taarifa iliyomtaja kuwa “ushahidi ulio hai kwamba mawazo ya mabadiliko yanaweza kutokea ndani ya jamii zilizokoseshwa makazi”. “Ameonyesha uwezo mkubwa wa rasilimali na umakini katika kuimarisha ubora wa elimu ya wakimbizi”, Grandi alisema.

Mire alizaliwa kusini mwa Somalia mwaka 1987, na aliishi katika kambi ya Dadaab iliyopo nchini Kenya miaka ya 1990 wakati familia yake ilipotoroka kutoka Qoryooley katika mkoa wa Lower Shabelle kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii