Korea Kaskazini imesema imefanikiwa kuweka satelaiti yake ya kwanza ya kijasusi kwenye anga ya juu ya dunia Jumanne jioni na kuapa kusafirisha nyingine kadhaa katika muda mfupi ujao.
Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA, limesema kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un alishuhudia uzinduzi huo kutoka kituo kilichoko Tongchang-ri kwenye pwani ya magharibi ya nchi hiyo.
Roketi iliyotumika ya Chollima-1 ilisafiri kufuata njia ya kawaida iliyopangwa na kuiweka kwa usahihi satelaiti hiyo ya upelelezi Malligyong-1 kwenye mzunguko wake saa kadha baada ya kufyetuliwa angani, shirika la habari la KCNA liliripoti.
Maafisa wa Marekani na Korea Kusini hawajathibitisha hadharani iwapo satelaiti hiyo ilifika kwenye mzunguko wa anga ya juu ya dunia lakini wamelaani safari hiyo kuwa ni uchochezi unaokiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.