Baraza la Waisalam Nchini, limeiomba Serikali kuondoa tozo za Ada ya Visima vya Maji kwenye Misikiti kwani zinahatarisha utekelezaji wao wa ibada kwa usahihi endapo watashindwa kuzimudu na hivyo kupunguza maana halisi ya Sala na Uislamu.
Ombo hilo, limetolewa na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Sheikh Nuhu Jabir Mruma mbele ya halaiki wakati wa baraza la maulid lilofanyika mkoani Dodoma na kuongeza kuwa Ibada ya Dini ya Kiislamu hutegemea uwepo wa maji kama nguzo mojawapo ya kukamilisha utaratibu kabla ya Sala.
Alisema, ” moja ya hitaji kubwa la msingi katika utekelezaji wa ibada kwa muislamu ni maji, na Misikiti mingi ama kwa nguvu zao au za wahisani wamechimba visima, huduma hii haikuwa na malipo, kwasasa baadhi ya Misikiti imeanza kutumia ankara na gharama ni kubwa, hali hii ikiendelea watashindwa kuendesha ibada kiusahihi, tunaiomba Serikali itoe msamaha wa Ada ya Visima.”
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuelekeza Katibu huyo kuandika barua na kuifikisha ofisini kwake, itakayoainisha mahitaji husika na misikiti inayotumia Visima ili waweze kushughulikia changamoto hiyo.