Serikali imesema Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
na Kati ni mojawapo ya wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia
vinavyowasababishia kushuka kwa ufanisi kwenye masomo yao, hivyo kupitia
Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto
(MTAKUWWA) wa mwaka 2017/18-2021/22 Serikali kwa kushirikiana na Wadau
wake inatekeleza Mpango wa uanzishaji wa Madawati ya Jinsia katika Vyuo
hivi ili kukomesha vitendo hivyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Dawati la Jinsia chini ya Mradi wa Our Right, Our Lives, Our Future
(03 plus) unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO ) Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) alisema Madawati hayo
yatasaidia kupambana na Ukatili wa Kijinsia vyuoni hivyo, yasimamiwe
kikamilifu yalete tija na yasiwe ya utendaji wa mazoea.
Amesema,
Serikali itasimamia kuanzia Vijijini hadi Taifa kuimarisha mifumo ya
kutokomeza ukatili wa kijinsia na amewaomba UNESCO kushirikiana na
Serikali ili huduma hii ifike kwenye vyuo vyote 512 nchini.
“Kuna
matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii na yanaongezeka siku
hadi ikiwemo vyuoni hivyo, huu ni wakati wa kuyatokomeza kwa kuweka
mikakati madhubuti ikiwemo Dawati la Jinsia kwenye kama ilivyoelekezwa
na Serikali” alisema Dkt. Gwajima.
Vielvile, Dkt Gwajima amesema,
Madawati hayo yanatakiwa kuwa Hai, madhubuti na yanayofanya kazi kwa
vitendo wakati wote kwa kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili kwa
kuwapatia huduma stahiki.
“Tutakuwa tunafanya ziara ya mara kwa
mara kutembelea madawati haya pia tutakuwa na mfumo wa kupima utendaji
wake ili isije ikawa tumefungua kwa mazoea yakakosa tija” alisisitiza.
Dkt. Gwajima.
Hata hivyo alisema, Serikali imetekeleza mambo
mengi katika kupambana na ukatili wa kijinsia mathalani kukuza uelewa wa
wananchi ambapo matukio 20,025 yameripotiwa mwaka 2020/21
ikilinganishwa na 18,270 mwaka 2019/20, Madawati ya Jinsia 420 yameundwa
kwenye Vituo vya Polisi na 153 kwenye Jeshi la Magereza, Kamati 18,186
za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zimeanzishwa nchini, vituo vya huduma
kwa wahanga vimeanzishwa kwenye hospitali 14, Sheria ya msaada kwa
wahanga na 1 ya mwaka 2017 imetungwa na mambo mengine mengi.
Naye,
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga, alisema
mradi wa ‘03plus’ utanufaisha Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam (UDSM) na
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na juhudi zitaendelea kupanua huduma hii
kwenye vyuo vingine nchini “Serikali ya awamu ya sita imejipanga
kikamilifu kuondoa hii changamoto ya ukatili wa kijinsia” alisema
Kipanga.
Katika uzinduzi huo Makamu Mkuu wa Chuo Profesa, William
Anangisye alisema mradi wa “03plus” una malengo matatu ambayo ni
kuondoa mimba za utotoni, kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi na
kutokomeza kabisa ukatili wa kijinsia katika vyuo vikuu. Pia alisema
mradi huo unalenga kutimiza malengo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kati.
Aidha
Mkurugenzi Mwakilishi wa UNESCO nchini Tirso Santos alisema, lengo la
kuleta mradi huo ni kutaka kuona wanafunzi wa vyuo vya juu wanasoma huku
wakijiamini “Wanafunzi wengi wa kike wanasoma bila ya kujiamini kwa
sababu ya kupata changamoto za ukatili wa kijinsia”alisema Santos.
Wakiongea
wakati wa hafla hiyo wanachuo Sauda Charled na Upendo Lugemdo, kutoka
Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam na Dodoma wameipongeza Serika na Wadau kwa
kushirikiana kutekeleza Mpango wa Dawati la Jinsia ambao wamesema
utakuwa mkombozi kwao.