Wafanyakazi wa uwanja wa ndege nchini Mauritius wamekuta mtoto mchanga wa kiume aliyetelekezwa kwenye chombo cha kuhifadhia taka ndani ya choo cha ndege ya Air Mauritius.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 20 kutoka Madagascar anayeshukiwa kujifungua kwenye ndege, alikamatwa. Ndege ya Air Mauritius, iliyowasili kutoka Madagascar, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seewoosagur Ramgoolam tarehe 1 Januari.
Maafisa wa uwanja wa ndege walimkuta mtoto huyo wakati wanafanya ukaguzi wa kawaida wa forodha. Walimkimbiza mtoto huyo katika hospitali ya umma kwa matibabu.
Mwanamke anayeshukiwa kuwa mama wa mtoto huyo ambaye awali alikana kuwa ni wake, alifanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ambao ulithibitisha kuwa alikuwa amejifungua.
Aliwekwa chini ya uangalizi wa polisi katika hospitali hiyo na wote yeye na mtoto wanaendelea vizuri.
Mwanamke huyo wa Madagascar, ambaye alifika Mauritius kwa kibali cha kufanya kazi cha miaka miwili, atahojiwa baada ya kuachiliwa kutoka hospitalini na kushtakiwa kwa kumtelekeza mtoto mchanga.