Waiba vifaa vilivyonunuliwa kwa tozo za miamala

Watu wanne wakiwemo viongozi wa Kijiji cha Shishani, Kata ya Shishani, Magu mkoani Mwanza, wanashikiliwa na polisi wilayani humo kwa tuhuma za wizi wa mabati 60 pamoja na vigae vilivyonunuliwa na serikali kwa fedha za tozo za miamala ya simu kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Shishani.

Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya cha Shishani kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Magu ikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Salum Kalli ikazungumza na wananchi ndipo likaibuka suala la wizi wa vifaa hivyo kama anavyoeleza Musa Masalu mkazi wa Kijiji hicho.

"Mimi nina uchungu sana, ninavyosema sikufichi wananchi wazuri sana wa Shishani isipokuwa viongozi wa hapa ni wabaya mno wameoza kabisa, yani imenuka kabisa Shishani hii hospitali imejengwa hii mavitu mengi sana yameibiwa mlinzi alisema nimeona fulani na fulani mheshimiwa diwani akakataa kabisa je hiyo inakuja kweli?," amesema mmoja wa wananchi

Suala la wizi wa vifaa hivyo vya ujenzi likamuibua Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Magu Fiderica Myovela, na kusema vifaa vyote vya miradi ya maendeleo vinapaswa kulindwa huku mwenyekiti wa kama ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ya Magu ambae pia ni Mkuu wa wilaya Salum Kalli, akasema atahakikisha wahusika wote wa wizi huo wanatiwa mbaroni huku akithibithisha wanne kushikiliwa.

"Mimi ndiyo Mkuu wa wilaya nilituma jeshi hapa wapo baadhi yenu wameshakamatwa si mnafahamu mengine hatutangazi siyo lazima, lakini tumewakamata zaidi ya watu wanne wako polisi taarifa zao zipo polisi na tutawafikisha mahakamani na lazima vile vitu walivyoiba watalipa na watarudisha," amesema DC KalliPata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii