Rais wa Angola Joao Lourenço kuapishwa kwa muhula wa pili

Rais wa Angola Joao Lourenço anaapishwa leo Alhamisi Septemba 15 mjini Luanda kwa muhula wa pili, baada ya ushindi mdogo wa chama chake katika uchaguzi wa wabunge wa mwezi Agosti, ambao matokeo yake yalipingwa upinzani.

Angola ilifanya uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi katika historia yake tarehe 24 Agosti. Katika nchi hii ya kusini mwa Afrika, hakuna uchaguzi wa rais na mtu anayechukuwa nafasi ya kwanza kwenye orodha ya watu waliowekwa na chama kilichoshinda katika chaguzi za ubunge anakuwa mkuu wa nchi moja kwa moja.

Chama cha Popular Movement for the Liberation of Angola (MPLA), madarakani tangu uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975, kilishinda uchaguzi kwa 51.17% ya kura, alama ya chini zaidi kuwahi kurekodiwa.

Chama cha kwanza cha upinzani, Umoja wa Kitaifa wa Uhuru (Unita), kilipata 43.95% ya kura.

Bw. Lourenço, 68, anatarajiwa kula kiapo wakati wa sherehe rasmi katika Uwanja wa Jamhuri, eneo la kihistoria katika mji mkuu ambapo mazishi ya kitaifa  ya mtangulizi wake na kiongozi wa zamani aliyekuwa na ushawishi mkubwa, rais wa zamani José Eduardo dos Santos, yaliandaliwa katikati ya wiki ya uchaguzi.

Viongozi kadhaa wa nchi na serikali wanatarajiwa kuhudhuria katika hafla hii, akiwemo Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Sousa.

Katika mkesha wa sherehe, Adalberto Costa Junior, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Unita, alibaini kwamba chama chake kitakubali wabunge wake watawazwe siku ya Alhamisi, baada ya kupinga kwa muda mrefu kutambua matokeo ya uchaguzi, yaliyogubikwa na "kasoro", amesema.

Unita ilipinga matokeo haya mahakamani, lakini rufaa yake ilikataliwa mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba, mahakama ya katiba ilibaini kwamba hakuna ushahidi unaoweka mashakani uchaguzi huo.

"Maafisa wengi wa polisi wengi mitaani"

Mitaa ya Luanda iko chini ya uangalizi mkali wa polisi leo Alhamisi, mwandishi wa shirika la habari la AFP amebainisha. Chama cha Unita kimeshutumu vikosi vya usalama vilivyosambazwa "nchini kote na vyenye silaha nzito" kwa kutaka "kuwatisha raia wanaokusudia kuandamana" siku ya kuapishwa "rais asiye na uhalali".

"Nitasalia nyumbani kesho, kuna maafisa wengi wa polisi mjini," Joao, mwanafunzi wa shule ya upili kutoka vitongoji vya Luanda, ambaye alitaja tu jina lake la kwanza, ameliambia shirika la habari la AFP.

Makundi ya kutetea haki za binadamu pia yametilia shaka haki ya uchaguzi. Wajumbe wanne kati ya 16 wa Tume ya Uchaguzi walikataa kutia saini matokeo ya mwisho. Waangalizi wa kigeni kutoka Afrika wameelezea "wasiwasi" kuhusu orodha za wapiga kura hasa.

Angola ambayo ni nchi tajiri wa maliasili, ni mojawapo ya nchi zisizo na usawa duniani. Mafuta yamewatajirisha watu walio karibu na dos Santos na nusu ya Waangola milioni 33 wanaishi chini ya mstari wa umaskini.

Bw. Lourenço alishangaza wengi mara alipochaguliwa kwa kuwafuta kazi viongozi wengi wa taasisi na makampuni pamoja na wakuu wa vyombo vya usalama, akiwalenga wale walio karibu na dos Santos na hasa binti yake Isabel, aliyeitwa "binti wa mfalme".

Ushindi ulipotangazwa, Bw. Lourenço aliahidi "mazungumzo na mashauriano" kwa muhula wake wa pili. MPLA ilipoteza thuluthi mbili ya wingi wa wabunge bungeni, ambayo hadi sasa imewezesha kupitisha sheria bila kuungwa mkono na chama kingine, ikiwa na viti 124 kati ya 220.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii