Samia ashangazwa na askari aliyesifia gongo

Rais Samia Suluhu Hassan ameshangazwa na kitendo cha askari polisi aliyevalia sare ya jeshi hilo akiisifu gongo.

Akizungumza leo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya kozi ya uofisa ya chuo cha taaluma cha polisi Samia amesema alikuwa hajui anamaanisha nini.

“Kiukweli nilishangazwa na ile video yani askari kwenye sare za kazi anaisifia pombe haramu na pale kuna raia sasa sijui alikuwa ana maana gani. “Clip kama hizi wengine tukiziona tunabaki tunasisimuka, mmmh haya bana sijui IGP na wewe uliiona na kama uliiona sijui yule bwana yuko wapi,”

Rais pia amelitaka jeshi la polisi kujipanga kikamilifu kuhakikisha usalama unatawala katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

“Furaha ya kumaliza mwaka isije kuleta misiba ndani ya nchi yetu, jeshi la polisi likasimame vyema na doria zifanyike kila mara kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika.

“Tumefanya kazi kubwa kupunguza makosa ya uhalifu mkubwa ambao ulitaka kuanza kuota mizizi lakini tumefanikiwa kuondoa,” amesema Rais Samia.

Amesema,”Yaliyobaki ni haya makosa madogo nayo tuyafanyie kazi kuyapunguza, hatuwezi kusema  tutamaliza ila tuhakikishe yanapungua kadiri ya uwezo wetu,”.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii