Bilionea pekee Afrika Mashariki anatoka Tanzania-Ripoti

Bilionea pekee wa Afrika Mashariki anatoka Tanzania, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kampuni ya utafiti ya New World Wealth and Henley & Partners inayosaidia watu wenye thamani ya juu kupata makazi au uraia kupitia uwekezaji.

Ripoti hiyo hata hivyo haikumtaja bilionea husika huku watu wengi zaidi wakiingia kwenye safu ya mamilionea wa dola. Ripoti ya Utajiri wa Afrika 2022 inaonesha kuwa Tanzania ina watu 2400 wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni1, Nation limeripoti.

Zaidi ya nusu ya mamilionea wa dola (1300) wanaishi katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam huku jiji hilo likiorodheshwa katika nafasi ya 12 kwa utajiri, huku raia binafsi wakiwa na utajiri wa dola bilioni 24.

Idadi ya mamilionea wa dola za Tanzania katika utafiti huo ni kubwa zaidi kuliko makadirio ya ripoti nyingine, ikionesha ugumu wa kufuatilia matajiri barani Afrika.

Ripoti ya Utajiri wa Afrika ya 2022 ilitokana na data iliyokusanywa na New World Wealth na pia hifadhidata ya Henley & Partners ya watu wenye thamani ya juu, inayojumuisha hasa watu wenye cheo cha mkurugenzi, Mkurugenzi Mtendaji, mwanzilishi na mshirika.

Afrika Kusini ina idadi kubwa zaidi ya mamilionea wa dola wakiwa 39,300 ikifuatiwa na Misri (16,900) na Nigeria (10,000), kulingana na ripoti ya kwanza ya utajiri na Henley.

Tanzania ilishika nafasi ya saba tena kwa kuwa na utajiri wa dola milioni 10 au zaidi. Tanzania ina watu 80 wa aina hiyo, nyuma ya Ghana (120) Morocco (220) Kenya (340) Nigeria (510), Misri (880) na Afrika Kusini (2,080). Tanzania imeorodheshwa ya sita kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ikiwa na utajiri wa angalau dola milioni 100, wanaojulikana pia kama mamilionea.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii