Watoto hatarini janga la ulawiti, ubakaji

Ni saa 2.00 usiku, kwenye kibanda cha kuonyesha video maarufu kwa jina la ‘kibanda umiza’ eneo la Semtema, Manispaa ya Iringa.

Katika kibanda umiza panafurika sana siku za mechi kubwa, ama za Ulaya au Simba na Yanga na zingine za ligi za hapa nyumbani.

Watoto wadogo baadhi wakiwa na miaka kati ya minne mpaka 12 ndio waliojaa kwenye kibanda hicho usiku.

Mwandishi wa habari hizo alijipenyeza na kuanza kuzungumza na watoto waliokuwepo, huku akijifanya kuwa anamtafuta mtoto mmojawapo.

“Namtafuta mtoto wangu,” nilisema baada kuingia kwenye kibanda hicho na kukutana na mhudumu.

“Ni nani, mtafute au huenda hajaja,” alisema mtoto mmoja.

Mwandishi aliendelea kuwadodosa baadhi ya watoto hao kwa nini wapo mahali hapo mpaka muda huo.

Mtoto mmoja alinijibu kuwa mama yake hayupo hivyo anamsubiri akiwa hapo.

Ukweli ni kwamba idadi ya watoto wanaoingia kuangalia sinema na michezo kwenye vibanda hivyo katika manispaa ya Iringa ni kubwa huku wazazi wakiwaacha.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa mkoani Iringa na maeneo mengine nchini, huku Jeshi la Polisi likiainisha chanzo kikubwa ni vibanda umiza.

“Inawezekana kabisa kuna wakati wanawawekea watoto picha za ngono na hapo huamua kuwarubuni ili wawafanyie ubakaji na ulawiti. Ni hatari sana,” alisema Jimson Sanga, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoani Iringa, Elizabeth Swai anasema wazi kuwa maeneo hayo ni hatari na lazima hatua zichukuliwe kunusuru watoto.

“Kihesa hasa Semtema ndiko kunakoongoza kwa matukio ya ukatili kwa watoto na matukio mengi ya ulawiti, tunaona kabisa vibanda umiza ndio chanzo,” anasema Swai.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoani Iringa, Sauda Mgeni alisema kulingana na takwimu za Jeshi la Polisi, matukio ya watoto yanayoripotiwa yamekuwa yakiongezeka. Mwaka 2020 kulikuwa na matukio 439 na mwaka jana kulikuwa na matukio 384 yaliyoripotiwa polisi.

Hivi karibuni, mtoto wa miaka 14 alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuwalawiti wenzake 19.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema watoto hao walikuwa wanakutana kwenye kibanda umiza kilicho katika eneo la Kihesa Kilolo.

“Huyu kijana alipohojiwa alisema alikuwa anawalawiti watoto wenzake wakati walipokuwa wanaenda kuangalia TV, mbinu aliyokuwa anaitumia ni kuwapa watoto hao pesa za kununulia vitu kama juisi, pipi na biskuti,” alisema Bukumbi.

Alidai kuwa mtoto huyo alikuwa anapewa pesa na bibi yake, aliwahonga wenzake ili atekeleze azma yake.

Awali, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kilolo, Elizabeth Lugenge alitoa taarifa polisi kuhusu watoto watatu waliolawitiwa.

Alisema watoto waliokuwa wamelawitiwa walikuwa wanasoma katika Shule ya Sekondari Igeleke, Manispaa ya Iringa.

“Watoto waliletwa kituoni wakiambatana na ofisa mtendaji huyo, baada ya mahojiano waliwataja watoto watano, hao watano wakawataja wengine watano na mtuhumiwa aliwataja wengine sita,” alisema Lugenge.

“Watoto wote walipopelekwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa ya Frelimo, walibainika kufanyiwa ulawiti. Mtuhumiwa alisema alianza kufanya hivyo tangu mwaka 2019.”

Tukio jingine; Mwalimu Anord Mlay alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kulawiti zaidi ya watoto 12 katika eneo la Semtema, Kihesa, Mjini Iringa.

Mlay, maarufu kwa jina la Big, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa.

Kama ilivyo kwa tukio la kwanza, watoto hao walikuwa wakienda kuangalia TV kwenye kibanda cha Mlay.

“Nilienda kuangalia TV akanionyesha video, ndio akasema twende kwenye pagale tukafanye hivyo hivyo,” alisema mtoto mmoja, akizungumza na Mwananchi.

Alisema baada ya kufanyiwa hivyo alipewa hela, lakini aliambiwa asiseme kwa mtu.

Mtoto huyo alisema hakuweza kusema nyumbani kwao wala kwa walimu wake shuleni mpaka alipotajwa na wenzake.

“Nilikuwa naumia, lakini nilikuwa naogopa sana kusema, kama ningesema angenipiga,” alisema mtoto huyo.

Mtoto mwingine aliyekuwa kwenye orodha ya watoto waliolawitiwa Semtema, mjini Iringa alisema walikuwa wanawekewa picha za utupu, kisha mwekaji picha hizo anawaambia wajaribu kufanya kama walivyoona.

Baadhi ya wazazi walisema maeneo ya kuangalia TV na michezo kwa watoto ni hatari zaidi kwa Manispaa ya Iringa kutokana na matukio hayo.

“Unajua wanawatishia watoto ndio maana hawasemi chochote, inaumzia sana,” alisema.

Diwani wa Viti Maalumu Kanda ya Kihesa, Askalina Lweve alisema alifanya ziara kwenye familia za watoto waliokumbwa na mkasa huo akabaini mmoja alikuwa ameumizwa kiasi cha kushindwa kutembea.

“Inasikitisha sana, kwa kweli hili tukio lilitibua moyo wangu, niliamua kukaa na hawa wazazi kujua kwa nini hawakugundua mapema?” alisema.

Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu alisema hali ni mbaya.

“Inabidi tuingie kazini kuwasaidia watoto wetu, ni tatizo kubwa sana,” alisema Msambatavangu.

Alisema japo dhamana ni haki ya kila mtuhumiwa, haikuwa rahisi kwa mtoto aliyelawiti wenzake 19 kuachiwa kutokana na usalama wake mtaani.

“Huko mtaani watu walishachukia, kwa hiyo ilibidi ashikiliwe polisi mpaka alipofikishwa mahakamani. Wananchi wangeweza kumuumiza kwa matukio hayo,” alisema Msambatavangu.

Mzazi wa mmoja wa watoto waliolawitiwa alisema alishtuka baada ya kwenda Hospitali ya Frelimo na kuambia mwanawe alifanyiwa hivyo zaidi ya mara moja.

Alisema mbali na Kihesa, maeneo mengine hatari kwa ukatili kwa watoto ni Mashine tatu na Ipororo.

“Idadi ya watoto wanaofanyiwa ukatili huu inazidi kuongezeka, jambo hili tunakemea sana,” alisema mzazi huyo.

“Nilienda kuangalia TV akanionyesha video, ndio akasema twende kwenye pagale tukafanye hivyo hivyo,” alisema mtoto mmoja, akizungumza na Mwananchi.

Alisema baada ya kufanyiwa hivyo alipewa hela, lakini aliambiwa asiseme kwa mtu.

Mtoto huyo alisema hakuweza kusema nyumbani kwao wala kwa walimu wake shuleni mpaka alipotajwa na wenzake.

“Nilikuwa naumia, lakini nilikuwa naogopa sana kusema, kama ningesema angenipiga,” alisema mtoto huyo.

Mtoto mwingine aliyekuwa kwenye orodha ya watoto waliolawitiwa Semtema, mjini Iringa alisema walikuwa wanawekewa picha za utupu, kisha mwekaji picha hizo anawaambia wajaribu kufanya kama walivyoona.

Baadhi ya wazazi walisema maeneo ya kuangalia TV na michezo kwa watoto ni hatari zaidi kwa Manispaa ya Iringa kutokana na matukio hayo.

“Unajua wanawatishia watoto ndio maana hawasemi chochote, inaumzia sana,” alisema.

Diwani wa Viti Maalumu Kanda ya Kihesa, Askalina Lweve alisema alifanya ziara kwenye familia za watoto waliokumbwa na mkasa huo akabaini mmoja alikuwa ameumizwa kiasi cha kushindwa kutembea.

“Inasikitisha sana, kwa kweli hili tukio lilitibua moyo wangu, niliamua kukaa na hawa wazazi kujua kwa nini hawakugundua mapema?” alisema.

Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu alisema hali ni mbaya.

“Inabidi tuingie kazini kuwasaidia watoto wetu, ni tatizo kubwa sana,” alisema Msambatavangu.

Alisema japo dhamana ni haki ya kila mtuhumiwa, haikuwa rahisi kwa mtoto aliyelawiti wenzake 19 kuachiwa kutokana na usalama wake mtaani.

“Huko mtaani watu walishachukia, kwa hiyo ilibidi ashikiliwe polisi mpaka alipofikishwa mahakamani. Wananchi wangeweza kumuumiza kwa matukio hayo,” alisema Msambatavangu.

Mzazi wa mmoja wa watoto waliolawitiwa alisema alishtuka baada ya kwenda Hospitali ya Frelimo na kuambia mwanawe alifanyiwa hivyo zaidi ya mara moja.

Alisema mbali na Kihesa, maeneo mengine hatari kwa ukatili kwa watoto ni Mashine tatu na Ipororo.

“Idadi ya watoto wanaofanyiwa ukatili huu inazidi kuongezeka, jambo hili tunakemea sana,” alisema mzazi huyo.

Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeamua kuandaa rasimu ndogo ya sheria kwa lengo la kupambana na ukatili wa watoto.

Ofisa Sheria wa Manispaa ya Iringa, Nasho Kayoka alisema sheria hiyo pia itawabana wazazi wasiotimiza wajibu wao kwa watoto.

“Mchakato huu ulianza mwaka jana na rasimu hii imetokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili hivyo tukaona hii itasaidia,” alisema.

Kayoka alisema bado wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwalinda watoto badala ya kuwaacha waendelee kufanyiwa ukatili.


Lweve, ambaye ni diwani wa Kihensa alisema wazazi na walezi wengi wapo bize kutafuta maisha na kusahau ulinzi kwa watoto wao.

“Fikiria mtoto analawitiwa tangu mwaka 2019, huna taarifa wala hujui lolote mpaka walimu waje kugundua? Tunaenda wapi jamani, hizo hela ambazo wazazi mnatafuta zitakuwa na maana gani wanenu wakiharibika?” alihoji Lweve.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Swai alisema shughuli za kutafuta kipato lazima ziende sambamba na suala la malezi, vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi.

“Ulinzi kwa watoto lazima uanzie nyumbani, kama nyumbani hakuko salama hali itakuwa mbaya zaidi,” alisema Swai ambaye ni mkuu wa dawati hilo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga alisema mbali na uzembe wa kuwaacha watoto wakizurura, ulevi kupindukia pia ni chanzo cha matukio hayo.

“Sinema na ulevi kupindukia ni hatari sana kwa makuzi ya watoto,” alisema Sanga.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shagembe alisema msingi wa matukio ya ulawiti hasa kwa watoto ni changamoto katika malezi kwa anayetenda au anayetendewa.

Alisema kwa anayetendewa inasababishwa na uangalizi duni wa wazazi, unaotokana na kukosa nafasi ya kukaa na mtoto kumdadisi.

“Kwa mfano tunapoishi na familia kubwa katika nyumba moja, kila mmoja huwa na tabia yake, mzazi atakwenda kazini anamuacha mtoto na wanafamilia, kama hatatenga

muda wa kumdadisi mtoto kujua anaishije kutwa ni ngumu hata kama anashawishiwa kufanyiwa vitendo hivyo,” alisema Shagembe.

Pia, alisema wazazi wengi hukosa muda na watoto kutokana na kukabiliwa na majukumu, hivyo kuiachia familia ambayo ndiyo inayohusika kuwaharibu.

Shagembe ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa), alisema matukio hayo hufanywa na watu wa karibu wa watoto hao kwa kuwa ndio wenye nafasi kubwa ya kuwafikia na kuwashawishi.

Kumwacha mtoto alale na mgeni, aliitaja kuwa moja ya tabia inayohatarisha usalama wa mtoto dhidi ya matukio ya ulawiti.

Alieleza familia nyingi hujenga imani na wageni kwa kufikiri unasaba nao na kutazama muonekano, bila kujiridhisha na tabia zao, huku akisema watoto wengi wanaharibiwa kwa imani hizo.

Kuhusu watoto wanaofanyiana wenyewe kwa wenyewe, alisema inatokana na pengine kuwahi kushuhudia au kufanyiwa, hivyo anamfanyia mwenzake kwa majaribio.

Alitaja uangalizi wa watoto, udadisi na kujenga urafiki nao ni mbinu muhimu za kubaini mapema iwapo mtoto atakaribia kufanyiwa vitendo hivyo.

Mhadhiri wa Ustawi wa Jamii, Dk Zena Mabeyo alitaja utandawazi kuwa moja ya sababu za matukio hayo.

“Anayeachiwa mtoto unakuta anaangalia aina fulani za video zinazomchochea kwa kuwa hana hela ya kupata mtu wa kutimiza haja zake, anajikuta akifanya kwa mtoto kwa kuwa hatatumia gharama,” alisema.

Februari 10, 2022, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi lilimkamata mwalimu wa mafundisho ya dini katika Kanisa la Katoliki Mpanda Mjini, Joseph John (27) akituhumiwa kuwalawiti watoto wanne.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi ACP, Ally Makame alisema mtuhumiwa ametenda kosa hilo maeneo tofauti kwa kuwalaghai watoto hao wamsindikize kwenda kufanya shughuli za biashara sehemu tofauti.

“Alikuwa anawabeba kwenye pikipiki yake baada ya kumaliza vipindi vyao vya masomo ya dini kisha kuwafanyia ukatili huo,” alisema Makame.

“Baada ya kumkamata tulimhoji akakiri kufanya hivyo, na baadhi ya watoto tuliowahoji wamekubali kufanyiwa.”

Machi 29, 2022 Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita lilimsaka mkazi wa Nyarugusu kwa tuhuma za kuwalawiti ndugu zake watatu wenye umri wa miaka 10 na mwingine minane.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alikiri kuwa kijana huyo (16) ambaye anajihusisha na shughuli za uchimbaji madini anatuhumiwa kuwalawiti watoto hao ambao ni watoto wa wajomba zake anaoishi nao kwa babu yao Kata ya Bukoli.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, watoto hao walidai kuwa, binamu yao huyo amekuwa akiwaingilia kinyume na maumbile kwa muda mrefu, lakini waliogopa kusema kutokana na kuwatisha kuwa atawaua.

“Usiku ukiingia kila mtu akiwa amelala anatuamsha na kutuambia tuvue nguo kisha anashusha suruali, anatuinamisha kwa zamu, akitoka kwangu anakwenda kwa mwingine hadi wote watatu, anapomaliza ndio analala,” alisema mmoja wa watoto hao.

Tukio lingine ni la Aprili 9, watoto wanane wa shule ya msingi Tembo Mashujaa, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamedaiwa kubakwa na kulawitiwa kwa nyakati tofauti na kijana mmoja.

Kati ya watoto hao, wanane ni wa kiume na mmoja wa kike ambao wana umri kati ya miaka minne hadi tisa.

Pamoja na kufanyiwa vitendo hivyo, inadaiwa watoto hao kufundishwa kufanya vitendo hivyo kwa wenzao na kuwekeana vitu visivyofaa sehemu za siri.

Mmoja wa wazazi wa watoto, Devotha Mgunya (si jina halisi) alisema walipigiwa simu na uongozi wa kamati ya shule na walipokwenda walielezwa tatizo lililowakuta watoto wao.

“Mtoto mmoja alipogundulika kuwa amefanyiwa kile kitu, alisema hayupo peke yake, kuna wenzake, akaanza kuwataja, wote wanasoma darasa moja. Walipohojiwa walikiri kufanyiwa vitendo hivyo na kijana ambaye yupo mtaani,” alisema.

Mtoto mwingine alimweleza mwandishi wa gazeti hili kuwa kutokana na kufanyiwa vitendo hivyo amekuwa akipata maumivu makali anapokwenda kujisaidia, lakini hakusema kwa kuwa alitishiwa kuuawa iwapo atamtaja ‘uncle’ anayewafanyia vitendo hivyo.

Alisema kijana anayedaiwa kuwafanyia vitendo hivyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20, alikuwa akiwadanganya kwa kuwapatia vindege, pipi na kucheza nao kwa kukimbizana.

Mwenyekiti wa kamati ya shule, Paul Joseph alipohojiwa alikiri kuwapo watoto wanane wanaodaiwa kulawitiwa.

Nilitafutwa ili kufanya kikao cha kujadili jambo hilo, hivyo tuliwaita wazazi wote na kuwahoji na kila mmoja anamtaja mtuhumiwa huyo huyo,” alisema Joseph.Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii