SERIKALI kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imezitaka kampuni za kubahataisha kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kulinda maadili na ustawi wa vijana, huku zikiongeza mchango wake katika maendeleo ya kijamii kupitia elimu, afya na michezo.
Wito huo umetolewa leo Novemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, James Mbalwe, akibainisha kuwa, ongezeko la kampuni zinazoendesha michezo ya kubahatisha linapaswa kwenda sambamba na manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania.
Aidha, Mkurugenzi huyo wa GBT amewataka washiriki wa michezo ya kubahatisha, hususan vijana, kushiriki kwa uwajibikaji na kwa kiasi, huku wakitambua umuhimu wa kutenga muda na rasilimali zao kwa ajili ya kazi, shughuli za uzalishaji na majukumu mengine ya kijamii.
“Kwa sasa tunaendelea kushuhudia ongezeko la wadau wengi wanaoanzisha kampuni za kubahatisha nchini ambao wanasaidia kuleta maendeleo ya michezo, lakini sambamba na hilo tunahitaji kuona ongezeko pia, kwenye mapato ya Serikali na huduma za jamii,”
“Kwa hiyo, tunawakaribisha BetSasa rasmi katika soko la Tanzania. Hata hivyo, tunatoa wito kwao na kampuni nyingine kuongeza tija ya shughuli zao kwa kurejesha kwa jamii kupitia kusaidia sekta za afya, elimu, michezo na maeneo mengine muhimu ya maendeleo,” amesema Mbalwe.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BetSasa, Jimmy Kenneth, amesema kuwa, kampuni hiyo imejipanga kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni, masharti na miongozo ya mamlaka zinazosimamia sekta hiyo.
“Uzinduzi wa BetSasa unaongeza idadi ya kampuni zinazoshiriki katika soko la michezo ya kubahatisha nchini, mafanikio ya biashara hii yanapaswa pia kupimwa kwa mchango wake halisi katika kulinda jamii na kuchangia maendeleo ya taifa letu, hivyo tutahakikisha tunajikita katika mlengo huo ili kuleta maendeleo zaidi.” ameeleza Kenneth.
Kadhalika, Kenneth ametaja kuwa, uzinduzi wa kampuni hiyo unaendana na kampeni inayoitwa “Kusanya Point, Usepe na Jetour”, ikilenga kuwapa wateja fursa ya kushinda zawadi, kuanzia fedha taslimu kila wiki hadi gari jipya.
“Promosheni hii imeandaliwa mahususi kwa ajili ya wadau na wateja wetu wote. Kupitia kampeni hii, tutakuwa tukiwazawadia washindi 50 fedha taslimu kila wiki, huku zawadi kubwa ikiwa ni gari jipya litakalotolewa kila baada ya miezi mitatu.” amesema Kenneth.