Romuald Wadagni ameshinda uchaguzi wa urais Benin

Nchini Benin, Romuald Wadagni ameshinda uchaguzi wa urais, baada ya kupata asilimia 94 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ya awali, kufuatia uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita.

Tume ya Uchaguzi imetangaza matokeo hayo, wakati huu raia wa nchi hiyo wakisubiri matokeo ya mwisho. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, asilimia 58.7 ya wapiga kura ndio waliojitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Wadagni ni mshirika wa karibu wa rais Patrice Talon aliyemaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, sasa anakabiliwa na kibarua cha kutekeleza ahadi alizotoa, kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na kuimarisha usalama, wakati huu Benin ikikabiliwa na tishio la wanajihadi.

Wachambuzi wa siasa, wanasema rais huyo mteule, anatarajiwa kuendeleza sera za mtangulizi wake, wakati huu akikabiliwa na changamoto nyingi likiwemo suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mpinzani wake mkuu Paul Hounkpe, amekubali  kushindwa na kumpongeza, Wadagni ambaye alikuwa Waziri wa Fedha kabla ya kuwania urais.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii