Nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo ameripotiwa kuanza mgomo wa kuichezea Al Nassr akionya kuwa endapo malalamiko yake hayatashughulikiwa, yuko tayari kuondoka katika klabu hiyo pamoja na Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa ujumla.
Ronaldo, anayelipwa takribani pauni 488,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.7) kwa siku, anadaiwa kuchukua hatua hiyo kutokana na hisia kwamba klabu yake haipati haki sawa ikilinganishwa na wapinzani wake wanaosimamiwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).
PIF inamiliki asilimia 75 ya hisa katika klabu nne kubwa za Saudi Pro League ambazo ni Al Nassr, Al Hilal, Al Ittihad na Al Ahli.
Taarifa zinaeleza kuwa Ronaldo anaamini PIF imekuwa ikionyesha upendeleo kwa Al Hilal, Al Ittihad na Al Ahli, huku Al Nassr ikiachwa nyuma katika mgao wa rasilimali na usajili wa wachezaji wakubwa.
Sintofahamu hiyo imeibuka muda mfupi baada ya Al Hilal kukamilisha uhamisho wa Karim Benzema kutoka Al Ittihad, hatua iliyokuja wakati Al Hilal ikiwa pointi moja tu nyuma ya Al Nassr kileleni mwa msimamo wa ligi.
Ronaldo anaamini uhamisho huo umeifanyika makusudi ili kuipa nguvu Al Hilal katika mbio za ubingwa na wakati huohuo kuipunguzia ushindani Al Nassr.
Aidha inaripotiwa kuwa Ronaldo analalamikia Kocha wa Al Nassr, Jorge Jesus kutopatiwa bajeti ya kutosha kutoka PIF ukilinganisha na makocha wa timu pinzani, ingawa taarifa zinaeleza kuwa dili la Benzema lilifadhiliwa na wawekezaji wa nje, si PIF moja kwa moja.
Hata hivyo hatua ya Ronaldo imezua mjadala mkubwa ndani ya Saudi Pro League, huku mustakabali wake na Al Nassr ukiendelea kuwa kitendawili endapo pande husika hazitapata suluhu ya haraka.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime