Ukraine Yakanusha Shambulio la Droni Dhidi ya Makazi ya Putin, Urusi Yazidi Kudai

Serikali ya Ukraine Jumanne imekanusha vikali madai ya Urusi kuwa ilihusika na shambulio la droni lililolenga moja ya makazi ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ikisema hakuna ushahidi wowote wa kuaminika na kwamba Moscow inalenga kupotosha juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kuonya kuwa Urusi inaandaa mazingira ya kufanya shambulio jipya dhidi ya mji mkuu Kyiv, akiwataka wakazi kuwa macho.

Urusi ilidai Jumatatu kuwa Ukraine ilirusha droni kuelekea makazi ya Putin yaliyoko katika eneo la Novgorod, kati ya Moscow na St Petersburg.

Jumanne, Kremlin ilisema tukio hilo linachukuliwa kama “kitendo cha kigaidi” na “shambulio binafsi dhidi ya Rais Putin”, ingawa ilikiri kuwa haiwezi kutoa ushahidi wa madai hayo kwa sababu droni zote zilidunguliwa kabla ya kufika shabaha.

Kremlin pia iliongeza kuwa jeshi la Urusi tayari limeamua “namna, wakati na mahali” pa kulipiza kisasi dhidi ya Ukraine.

Ukraine imesisitiza kuwa madai ya Urusi hayana msingi wowote wa ukweli, ikieleza kuwa licha ya kupita kwa takribani saa 24 tangu dai hilo litolewe, Moscow haijatoa ushahidi wowote.

“Takribani siku moja imepita na Urusi bado haijatoa ushahidi wowote wa kuaminika,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiga, kupitia mitandao ya kijamii.

Baada ya madai ya Urusi, viongozi wa Ulaya walionesha mshikamano wao na Zelensky, huku Poland ikisema suala hilo lilitarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa viongozi wa Ulaya baadaye Jumanne.

“Tunaisukuma mbele mchakato wa amani. Sasa uwazi na uaminifu vinahitajika kutoka kwa kila upande – ikiwemo Urusi,” alisema Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, kupitia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alizungumza na Putin Jumatatu, alielekeza lawama kwa Ukraine licha ya Kyiv kusema tukio hilo ni la kutungwa.

“Unajua ni nani aliyeniambia? Rais Putin, mapema asubuhi. Alisema ameshambuliwa. Hilo si jambo zuri,” alisema Trump.

“Ni jambo moja kushambulia katika vita, lakini ni jambo lingine kushambulia nyumba yake,” aliongeza.

Urusi haijasema Putin alikuwa wapi wakati wa tukio hilo linalodaiwa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii